Kupungua vifo Ukimwi, kifua kikuu, malaria, tujipongeze, tusishangilie

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:48 AM Mar 22 2024
Kifo.
PICHA: INDIA TODAY
Kifo.

Ni kweli kabisa hata kwa macho tu na utafiti usio wa kitaalamu, inaonekana kuwa vifo vya magonjwa ya malaria, Ukimwi na kifua kikuu maarufu TB vimepungua.

Ni kwa sababu hata wagonjwa wake wamepungua sana. Sasa hivi hata mitaani kunyoosheana vidole kwamba, 'yule anao', hakuna tena.

Miaka ya nyuma tulikuwa na ndugu, rafiki na jamaa ambao baadhi walikuwa wakiugua ya ukiulizia utaambiwa ana maambukizo ya ugonjwa wa ukimwi, ingawa haisemwi hadharani.

Watu tumeunguza sana ndugu, rafiki na jamaa zetu na tumezika sana. Kwa sasa unaweza kukaa kwa muda mrefu kukawa hakuna ndugu, jamaa au rafiki ambaye ukaambiwa ana tatizo hilo.

Hiyo ni kuthibitisha kuwa maambuziki ya ugonjwa wa Ukimwi yamepungua. Kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ni kwamba ugonjwa wa Ukimwi uliua watu 25, 000 mwaka 2021, lakini idadi ilipungua hadi kufikia 22,000 mwaka 2023.

Waziri huyo alitoa takwimu hizo akielezea miaka mitatu ya kuwa madarakani, Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wa malara, alisema 2021, iliua watu 1,882, lakini 2023 walipungua hadi, 1,540, wakati kifua kikuu 2023 kiliua watu 18,000, ukilinganisha na wagonjwa 26,800 waliokufa, 2023.

Kuna takwimu na uhalisia wa ndani ya jamii. Kama ilivyo kwa Ukimwi unaoonekana kwa sasa umepungua, hivyo hivyo kwa malaria na kifua kikuu.

Sasa unaweza kukaa hata mwaka mzima, hujasikia ndugu, jamaa au rafiki siyo tu amekufa kwa kifua kikuu, bali hata kuugua.

Miaka ya nyuma ilikuwa ni jambo la kawaida, kukuta ndani ya jamii kuna wagonjwa kibao wa kifua kikuu.

Nimeshuhudia jirani yangu akiwa anakwenda kumchukulia ndugu yake dawa Hospitali ya Mwanyamala, Dar es Salaam, ambaye alikuwa hawezi hata kunyanyuka kitandani, akiwa amedhohofu kwa kutafunwa na kifua kikuu.

Mwezi mmoja tu baada ya kunywa dawa, hali ya mgonjwa ikawa vizuri akainukia na kuanza mwenyewe kwenda kunywa au kuchukua dawa.

Mara ya pili tena nikashuhudia mtoto mdogo tu, mwenye miaka saba akiwa anaumwa ugonjwa huo, ingawa naye baadaye alipona baada ya kunywa dawa.

Hiyo inakuonyesha kuwa magonjwa hayo yalikuwa tishio mno miaka kadhaa nyuma, lakini tunaishukuru serikali kuwa inapungua kila miaka inavyozidi kusonga mbele.

Sasa hivi ndani ya familia, ndugu jamaa, ukisikia mgonjwa amelazwa, basi kaanguka na bodaboda, ajali ya gari, presha, sukari, kiharusi, na hata vifo chanzo ni hayo au mengine yanayofanana hayo na mengi ni yale yasiyo ya kuambukiza.

Na hii imetahadharishwa pia na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, juu ya ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza, akisema tathmini inaonyesha mpaka kufikia mwaka 2030, nchi za Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwamo Tanzania, zitakuwa zimekumbwa na magonjwa hayo kwa asilimia 70.

Tunamshukuru Rais Samia kwa kusimamia vyema sekta ya afya kiasi cha kila mwaka wagonjwa wanapungua na inawezekana huko mbele wakapungua zaidi, au kumalizika kabisa.
 Hata hivyo, wakati serikali ikifanya kazi yake, wananchi wakati wakijipongeza kwa familia zao kuwa salama, lakini wasishangilie kupitiliza, badala yake wasiiachie serikali mzigo wote.

Umakini uendelee kuongezeka, watu waache ngono zembe, watumie vifaa kama kondomu ili kutoeneza magonjwa ya zinaa, waendelee kufyeka nyasi ndefu na kuweka mazingira safi ili kupunguza ugonjwa na vifo vinavyotokana na malaria.

Madirisha makubwa yenye mwanga yanayoingiza hewa safi, kutokukaa sehemu zenye mkusanyiko wa watu wengi bila sababu maalum, kunaepusha uwezekano wa kupata ugonjwa wa TB.