RC azuia uhamisho walimu, awapa maagizo wakurugenzi

By Jaliwason Jasson , Nipashe
Published at 04:33 PM Mar 19 2024
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga
PICHA: Dar24
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amezuia uhamisho wa walimu wa msingi na sekondari kufanyika katika wilaya zote mkoani kwake.

Pia amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri kuwahamisha mjini walimu walioko kwenye shule zenye idadi kubwa ya walimu, kupelekwa shule za vijijini na pembezoni, ambazo zinakabiliwa na upungufu wa walimu.

Ametoa agizo hilo mwishoni mwa wiki, wakati akifungua kikao cha kamati ya ushauri cha mkoa huo.

"Nataka kuwepo na msawazo wa walimu, maana kada hii inakuwa na uhamisho mwingi mno. Wanajifanya kuwa na matatizo ya kiafya," amesema Sendiga.

Aidha, amesema watumishi wa umma wanapaswa kufanya kazi mahali popote, ila walimu na wauguzi wana haki ya kukaa popote ili wawahudumie wananchi inavyotakiwa.

Katika hatua nyingine, Katibu Tawala Msaidizi, Sekretarieti ya Mkoa wa Manyara, anayeshughulikia Uratibu na Mipango, Lusungu Mwilongo, amewasilisha Mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Mwaka mpya wa fedha 2024/25, ambayo Manyara itatumia Sh. bilioni 278.8

Mwilongo, amesema vipaumbele vyao vitakuwa ni amani na utulivu, kuboresha huduma za kijamii, ukamilishaji wa miradi viporo, ukusanyaji wa mapato na uchaguzi wa serikali za mitaa.

Wakati huo huo, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Babati (BAWASA), ikipanga kutumia Sh. bilioni 25 kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 80 hadi asilimia 95.

Amesema Wakala wa Maji na Usambazaji wa Maji Vijijini (RUWASA), imepanga kutumia Sh. bilioni 15.8, ambapo watatekeleza miradi 36 inayoendelea na miradi miwili mipya.