MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera, Devotha Daniel, ametoa msaada wa Sh. milioni 1 kwa mtoto Grecseous Raphael mwenye umri wa miezi minne, mkazi wa Kata ya Kihanga, Wilaya ya Karagwe, anayesumbuliwa na uvimbe kichwani ili kumwezesha kufikishwa Hospitali ya Rufani Bugando kwa ajili ya upasuaji.
Mbali na msaada huo wa fedha, mbunge huyo pia ameahidi kugharamia bima ya afya kwa familia nzima ya mtoto huyo ili waweze kupata huduma za matibabu kwa urahisi wanapohitaji, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za rais za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.
Ameeleza kuwa msaada huo ni sehemu ya kuendelea kusambaza tabasamu kwa wananchi kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayotarajiwa kufanyika mwezi Machi kila mwaka, na kwamba dhamira yake ni kuwatumikia wananchi kwa vitendo na kuwagusa wenye mahitaji maalum katika jamii.
“Nilipata taarifa za mtoto huyo kupitia matangazo ya redio Mama wa mtoto alikuwa akiomba msaada kwa wasamaria wema, jambo lililonigusa na kuamua kufika moja kwa moja kwa familia hiyo kujionea hali halisi,” amesema Devotha.
Mama wa mtoto huyo, Swaumati Sijaji, amemshukuru mbunge huyo kwa kuwafariji na kutoa msaada utakaomsaidia mtoto wao kufikishwa Bugando kwa matibabu.
Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Karagwe, Georgiana Mkapapa, amesema hatua hiyo inaonesha namna mbunge huyo alivyo karibu na wananchi wake na kuwataka kuendelea kumuunga mkono katika jitihada zake za kuwaletea maendeleo.

© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED