WIMBI la vurugu limezuka nchini Mexico baada ya anaedaiwa kuwa ni mlanguzi mkubwa wa dawa za kulevya nchini humo kuuawa katika operesheni ya kumkamata iliyohusisha idara ya ujasusi ya Marekani.
Mlanguzi huyo Nemesio Oseguera Cervantes, anayejulikana kama "El Mencho", alikuwa kiongozi wa genge la dawa za kulevya la ‘Jalisco New Generation’ (CJNG) na alifariki baada ya kujeruhiwa vibaya katika mapigano kati ya wafuasi wake na jeshi jana.
Wizara ya Ulinzi ya Mexico, imeeleza kuwa katika mapigano hayo wafuasi wanne wa genge hilo waliuawa wakati wa operesheni hiyo katika mji wa Tapalpa, katika jimbo la Jalisco, na wanajeshi watatu pia walijeruhiwa.
Kutokana na hali hiyo kumeshuhudiwa vurugu katika majimbo kadhaa, huku CJNG ikifunga barabara kwa magari yanayoungua. Na kwamba Jumapili nzima, kulikuwa na ripoti za watu wenye silaha mitaani huko Jalisco na kwingineko.
Gavana wa Jalisco, Pablo Lemus Navarro, alitangaza hali ya hatari katika jimbo la Guadalajara, akisimamisha usafiri wote wa umma na kufuta matukio ya halaiki na shule kufungwa.
Watalii waliozungumza na Reuters waliuelezea mji wa mapumziko wa Puerto Vallarta, Jalisco, kama ‘eneo la vita.’
Vizuizi vya barabarani takriban 250 viliwekwa kote nchini humo wakati wa machafuko, huku 65 vikiwa Jalisco.
Maduka yaliteketezwa kwa moto na takriban matawi 20 ya benki yalishambuliwa katika vurugu hizo.
Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum amesema maofisa wa majimbo na shirikisho wamedhibiti vurugu hizo, akiwahimiza watu kuwa watulivu.
Sheinbaum aliongeza kuwa "katika sehemu nyingi za nchi, shughuli zinaendelea kama kawaida".
Mashirika kadhaa ya ndege yamefuta safari za ndege kwenda Jalisco, ikiwa ni pamoja na Air Canada, United Airlines na American Airlines.
Marekani imewaonya raia wake kujificha katika majimbo matano: Jalisco, Tamaulipas, maeneo ya Michoacán, Guerrero na Nuevo Leon.
Inadaiwa kuwa El Mencho, ofisa wa zamani wa polisi mwenye umri wa miaka 59, aliendesha shirika kubwa la uhalifu linalohusika na usafirishaji wa kiasi kikubwa cha kokeini, methamphetamine na fentanyl kwenda Marekani.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliahidi zawadi ya dola milioni 15 sawa na takribani (Sh. Bilioni 38) kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa El Mencho.
BBC,RFI
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED