Milioni 361.5 kukarabati chumba cha upasuaji Ocean Road

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:00 PM Feb 23 2026
Milioni 361.5 kukarabati chumba cha upasuaji Ocean Road
Picha: Mpigapicha Wetu
Milioni 361.5 kukarabati chumba cha upasuaji Ocean Road

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Diwani Msemo, amesema msaada wa zaidi ya Sh milioni 361.5 uliotolewa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa ajili ya ukarabati wa chumba cha upasuaji na ununuzi wa vifaa tiba, utaleta faraja na matumaini mapya kwa wagonjwa wa saratani nchini.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo jijini Dar es Salaam leo Februari 23, 2026, Dk. Msemo amesema uboreshaji huo unakwenda kujibu hitaji la muda mrefu la taasisi hiyo.

“Kilichofanyika leo kinaleta majibu ya takribani miaka 30 iliyopita. Chumba hiki cha upasuaji kilipaswa kuwepo tangu mwaka 1996. Tunashukuru kwa kuungana na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kupeleka furaha kwa wananchi,” amesema.

Ameongeza kuwa uwekezaji huo una umuhimu mkubwa kwa kuwa utaiwezesha ORCI kuwa na chumba cha kisasa cha upasuaji kwa wagonjwa wa saratani, sambamba na vifaa tiba vya kisasa, hatua itakayoboresha huduma na kupunguza adha kwa wagonjwa.

Kwa upande wake, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama wa PSSSF, Omega Ngole, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu Fortunatus Magambo, amesema uamuzi wa kutoa msaada huo ulifikiwa baada ya ziara ya tathmini kubaini kuwa taasisi hiyo haina chumba cha upasuaji kinachojitegemea kwa wagonjwa wa saratani.

Amefafanua kuwa kati ya fedha hizo, Sh milioni 197,027,956 zitatumika kukarabati chumba cha upasuaji, huku Sh milioni 164,491,270 zikitengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.

“PSSSF inajisikia faraja kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya afya. Mfuko unahudumia wananchi wengi, wakiwemo wanachama wetu, hivyo ni muhimu kurudisha kwa jamii,” amesema.

Ameongeza kuwa msaada huo umetolewa kupitia sera ya uwekezaji kwa jamii (CSI) chini ya kaulimbiu ya #PSSSFKaribunaJamii, akieleza kuwa Watanzania wengi, wakiwemo wanachama na wastaafu, watanufaika na maboresho hayo ya huduma za saratani.