Maji yaleta fursa mpya Kasulu

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 06:27 PM Feb 20 2026
Maji yaleta fursa mpya Kasulu
Picha:Mpigapicha Wetu
Maji yaleta fursa mpya Kasulu

Kukamilika kwa Mradi wa Maji wa Miji 28 kunatarajiwa kunusuru maisha ya wananchi wa Mji wa Kasulu kwa kuwapatia maji safi na salama karibu na makazi yao, kupunguza magonjwa yatokanayo na maji na kuongeza tija ya kiuchumi katika jamii.

Hayo yalibainishwa leo na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kasulu, Samwel Kayombo, wakati akieleza maendeleo ya mradi huo mbele ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenan Kihongosi.

Kayombo amesema Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inatekeleza mradi huo chini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP 2006–2025), ukihusisha Mji wa Kasulu mkoani Kigoma. 

Mradi ulianza Aprili 11, 2023 na unatarajiwa kukamilika Julai 10 mwaka huu, ukitekelezwa na Megha Engineering and Infrastructure Ltd chini ya usimamizi wa WAPCOS Ltd kwa gharama ya Dola za Marekani 15,071,988 sawa na takribani Sh bilioni 34.67. Unatarajiwa kuhudumia wakazi 187,434 katika kata 12.

Amesema mradi unahusisha ujenzi wa chanzo cha maji katika Mto Ruchugi chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 16 kwa siku, kituo cha kutibu maji chenye uwezo wa lita milioni 15 kwa siku, matenki mawili ya Kumnyika (lita milioni 2) na Rusunwe (lita 500,000) pamoja na mtandao wa mabomba. 

Utekelezaji wa jumla umefikia asilimia 57 huku baadhi ya kazi kama ulazaji wa mabomba makazi ukisubiri kuwasili kwa vifaa.

Hata hivyo, Kayombo ametaja changamoto za kuchelewa kwa vifaa vinavyoagizwa nje ya nchi, uwepo wa mwamba mgumu katika eneo la mradi na uchelewaji wa nondo za ujenzi wa tenki la Kumnyika. 

Amesema Mamlaka inaendelea kumhimiza mkandarasi kuhakikisha vifaa vinafika kwa wakati ili mradi ukamilike kwa mujibu wa ratiba na malengo ya Serikali ya kuboresha huduma ya maji.

Naye Kihongosi baada ya kukagua mradi huo amesema ni ajenda ya CCM ya kutatua changamoto ya maji nchini na akampongeza Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara ya Maji na wataalamu wa mkoa kwa usimamizi mzuri. 

Ameagiza mkandarasi kuongeza kasi ili mradi ukamilike Julai 10 bila kuongezewa muda, akisisitiza kuwa wananchi wa Kasulu wanahitaji maji safi na salama, huku Serikali ikilenga kufikia upatikanaji wa maji vijijini kwa asilimia 85 na mijini kwa asilimia 95 ifikapo 2025–2030.