Mamlaka yatoa mafunzo ikionya matumizi holela ya dawa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:25 PM Feb 23 2026
news
Picha Da
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Gabriel Mashauri akizungumza na wakaguzi wa dawa mkoa wa Mwanza, wakati akifungua mafunzo ambayo yamefanyika wilayani Ilemela, leo Jumatatu. Picha na Damian Masyenene

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Mashariki, imeendesha mafunzo kwa wakaguzi kutoka halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza ili kuwajengea uelewa, ikiwa ni jitihada za kuhakikisha jamii haiathiriki na matumizi holela ya dawa yanayosababisha usugu, pamoja na zile zenye asili ya kulevya.

Mafunzo hayo yamefanyika leo wilayani Ilemela, mkoani Mwanza, yakilenga kufundisha wakaguzi angalau watatu katika kila halmashauri ili kuwaongezea ujuzi wanapotimiza majukumu yao.

Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki, Aggrey Muhabuki amesema wakaguzi hao wamefundishwa mbinu mbalimbali za kikaguzi, miiko, na maaidli ya ukaguzi, njia za ukaguzi, na sayansi ya utoaji wa madhara yatokanayo na matumizi ya dawa.

Vilevile, wameelimishwa kuhusu muongozo wa utunzaji sahihi wa dawa na vifaa tiba, na namna ya udhibiti usambazaji na utunzaji wa dawa na tiba zenye asili ya kulevya.

“Tunapofanya kaguzi hizi katika ngazi za halmashauri huwa tunawashirikisha wakaguzi hawa, na tunakuwa na vipindi kama hivi tunawaita na kuwafundisha kuhakikisha kwamba kulingana na matakwa ya uhitaji wa sheria na kanuni tunawanoa mara kwa mara ili wafanye kazi zao vizuri,” amesema Muhabuki.

Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Mashariki, Aggrey Muhabuki akizungumza leo mkoani Mwanza wakati wa mafunzo kwa wakaguzi wa dawa. Picha na Damian Masyenene
Amesema baada ya mafunzo hayo wanatarajia ufanisi katika shughuli zao kwani TMDA inahudumia halmashauri 23 katika kanda hiyo, hivyo uwepo wa wakaguzi hao wenye uelewa wa kutosha itakuwa ni msaada mkubwa katika kuilinda jamii.

“Tunatarajia ufanisi uwepo zaidi, tunapokuwa na matukio au taarifa za uwepo wa dawa duni na bandia kwenye soko basi watusaidie pale ambapo tunakuwa hatujafika kwenye haya maeneo,” amesema Muhabuki.

 Naye, ofisa kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Ziwa, Jafari Mtepa, amesema wanashirikiana na TMDA katika kuzuia dawa tiba zenye asili ya kulevya kuhakikisha dawa hizo zinatumika vizuri kwa utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria.

1
“Watu wengi kwa sababu huwa hawafahamu na wanaziona hizi dawa kama za binadamu lakini ukizitumia vibaya zinakusababishia matatizo kama dawa za kulevya zingine. Tunashirikiana na TMDA kuhakikisha uingizaji wa dawa unafuata taratibu, na matumizi yanakuwa ni sahihi ili yasiwaletee shida wananchi na jamii kwa ujumla,” amesema Mtepa.

Mmoja wa wakaguzi walioshiriki mafunzo hayo, Glory Mbuya ambaye ni Fundi Sanifu Dawa Wilaya ya Ilemela, ameshauri wananchi kuzingatia cheti wanachopewa na madaktari baada ya vipimo ili kununua dawa, kuliko kununua dawa kwa mazoea.

“Baadhi ya maduka ya dawa na vifaa tiba wanaficha hizi dawa mnappokwenda kukagua hazionekani lakini mteja akija wanazifuata wanakokuwa wamezificha, hivyo kupitia elimu tuliyoipata hapa tunakwenda kuongeza umakini zaidi katika kaguzi zetu,” amesema Mbuya.