Ado Shaibu aahidi 'kuwasha moto' bungeni kuwatetea wapigakura wake

By Stevie Chindiye , Nipashe
Published at 02:17 PM Feb 23 2026
Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu.

Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu, ameahidi kuendelea “kuwasha moto” bungeni kwa kuibua hoja nzito zenye maslahi kwa wananchi wake, zikiwemo ujenzi wa Chuo Kishiriki cha Sokoine Suwa, ujenzi wa Reli ya Kusini katika mikoa ya Mtwara na Ruvuma, pamoja na kufuatilia kwa karibu ufufuaji wa kiwanda cha kubangua korosho kilichosimama baada ya mwekezaji kuvunja mkataba.

Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara wa mrejesho wa siku 100 za uongozi wake tangu aapishwe, uliofanyika katika viwanja vya Baraza la Idd mjini Tunduru, Ado alisema ataendelea kuishinikiza Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo itakayochochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.

Alieleza kuwa ujenzi wa Reli ya Kusini utafungua fursa pana za kiuchumi kwa kuunganisha mikoa ya Mtwara na Ruvuma, sambamba na kuziunganisha na nchi jirani za Msumbiji na Malawi. Kwa mujibu wake, miundombinu hiyo itarahisisha usafirishaji wa mazao, kuongeza biashara za mipakani na kuinua kipato cha wananchi.

Kuhusu kiwanda cha kubangua korosho, mbunge huyo alisema suala hilo si la bahati mbaya bali ni ahadi ya Rais, hivyo jukumu lake ni kuikumbusha Serikali kuhakikisha ahadi hiyo inatekelezwa. Aliongeza kuwa ataiomba Serikali kuviwezesha vyama vikuu vya ushirika vya wakulima wa Tunduru (TAMCU) na AMCOS kwa kuwapatia mitaji ili waweze kusindika na kubangua korosho ndani ya nchi, badala ya kuuza mazao ghafi yanayonyima wananchi thamani na ajira.

Katika kipindi chake cha siku 100, Ado alisema ameuliza maswali ya msingi na ya nyongeza kuhusu mradi wa maji wenye thamani ya Sh bilioni 3.4, fidia kwa wahanga wa matukio ya tembo, pamoja na hoja ya kugawa Tunduru ili kuwa na halmashauri mbili kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi.

Alifafanua kuwa Tunduru ina eneo la zaidi ya kilometa za mraba 18,000, kata 39 na wakazi zaidi ya 400,000, hivyo kugawanywa kwake kutarahisisha utoaji wa huduma za kijamii na usimamizi wa maendeleo.

Akizungumza kwa hisia kali, mbunge huyo alisema katika kipindi kifupi ameanza kuchukua hatua za moja kwa moja kusaidia wananchi, ikiwemo kutoa gari lake binafsi kwa ajili ya kubeba wagonjwa na miili ya marehemu, huku akitenga Sh milioni moja kila mwezi kwa ajili ya uendeshaji wake. Pia amepokea Sh milioni 70 za Mfuko wa Jimbo zinazotarajiwa kupangiwa matumizi baada ya vikao husika kukamilika.

Kwa upande wao, wananchi waliibua kero mbalimbali zikiwemo ubovu wa barabara, malipo ya matibabu kwa wazee, wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, uhaba wa watumishi katika shule na hospitali, miundombinu chakavu ya hospitali, pamoja na madai ya rushwa katika baadhi ya vituo vya polisi.

Kero nyingine zilizotajwa ni pamoja na uhitaji wa maeneo ya kilimo, mikopo kwa wachimbaji wadogo, ujenzi wa matuta katika maeneo ya mikusanyiko kama shule, pamoja na ujenzi wa soko na stendi za kisasa zenye hadhi.

Mbunge huyo aliwahakikishia wananchi kuwa atayachukua yote yaliyowasilishwa na kuyafanyia kazi kwa kuyapeleka katika vyombo vya maamuzi, akisisitiza kuwa dhamira yake ni kuona Tunduru inapiga hatua za haraka za maendeleo.