RAIA wa Uganda Vicky Ajok aliyekuwa akifanya kazi za ndani huko nchini Syria amehukumiwa kifo baada ya kukutwa na hatia ya kumuua aliyekuwa muajiri wake raia wa Syria.
Wakati hukumu hiyo ikitarajiwa kutekelezwa Februari 28, mwaka huu, Shirika la Migrant Workers Voice Uganda limewahimiza maofisa jijini Kampala kuzungumza na wenzao wa Syria ili kusimamisha utekelezaji wa hukumu hiyo dhidi ya Vicky.
Imeelezwa kuwa Vicky alihukumiwa kwa kumuua mwajiri wake mwenye umri wa miaka 87, Huda Shaarawi, ambaye ni mwigizaji maarufu wa tamthilia za televisheni nchini Syria. Tukio hilo lilitokea mwezi uliopita katika mji mkuu wa Syria, Damascus.
Kwa mujibu wa ripoti, Vicky alimpiga mwajiri wake kwa kitu kizito wakati wa mabishano, na kusababisha majeraha mabaya. Inasemekana alikimbia eneo la tukio lakini baadaye akakamatwa.
Katika taarifa ya kukiri ambayo ilisambazwa katika vyombo vya habari vya ndani, inasemekana alitaja unyanyasaji wa muda mrefu na mishahara isiyolipwa kama sababu zilizosababisha tukio hilo.
Video iliyochapishwa kwenye chaneli ya Uganda ya New Vision YouTube inamwonyesha Vicky akiwa katika chumba akiwa amezungukwa na watu wanaoaminika kuwa maofisa wa Syria, akionyesha jinsi alivyofanya shambulio hilo kabla ya kulia na kuomba msamaha.
Serikali ya Uganda bado haijatoa kauli yoyote kuhusu jambo hilo.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED