Kaya 92 Msomera zaathiriwa na mvua

By Hamida Kamchalla , Nipashe
Published at 02:39 PM Feb 23 2026
Kaya 92 Msomera zaathiriwa na mvua
Picha:
Kaya 92 Msomera zaathiriwa na mvua

Kaya 92 zimeathiriwa na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha usiku wa kuamkia leo katika Kijiji cha Msomera, wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Mvua hiyo iliyodumu kwa takribani saa mbili imesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu na mali za wananchi. Mbali na nyumba 92 kuathirika, madaraja matatu pia yameharibika, hali iliyokatiza mawasiliano katika baadhi ya maeneo.

Kwa upande wa taasisi za umma, Mahakama ya Mwanzo, Kituo cha Afya na jiko la Shule ya Sekondari Msomera zimepata madhara, huku taasisi za dini zikiathirika baada ya makanisa matatu kuezuliwa mapaa.

Akitoa taarifa ya tathmini ya awali ya uharibifu huo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, amesema kwa sasa mahitaji ya dharura ni mabati 1,000 ili kurejesha hali ya makazi kwa wananchi walioathirika.

“Kwa tathmini ya haraka tuliyofanya, wananchi wote walioathirika wanahitaji mabati 1,000 ili kurudisha mapaa yao kama ilivyokuwa awali,” amesema Nyamwese.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Batilda Buriani, amezielekeza mamlaka zinazohusika na miundombinu ya barabara na umeme kuhakikisha huduma hizo zinarejeshwa kwa haraka ili kupunguza adha kwa wananchi.

Aidha, ametoa pole kwa wahanga wote na kuwataka kuzingatia uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti na kurejesha uoto wa asili, akisisitiza kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zinaongezeka na zinahitaji hatua za pamoja za kukabiliana nazo.

“Mabadiliko ya tabianchi yanakuja na madhara mengi. Wajibu wetu ni kupanda miti na kuepuka ukataji holela,” ameasa.