Suala la rushwa miungu watu utumishi umma lifikie tamati

Nipashe
Published at 10:27 AM Jul 19 2024
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia.
Picha: Maktaba
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia.

UTUMISHI wa umma ni kuwatumikia watu. Huu ni msemo ambao umekuwapo enzi na enzi katika utumishi wa umma ukimaanisha kwamba mtu anapoingia katika kada hiyo, wajibu wake mkubwa ni kutoa huduma kwa wananchi kulingana na eneo alilopangwa kufanya kazi.

Tangu serikali ya awamu ya kwanza, ilisisitizwa kuwa watumishi wa umma katika ngazi zote, wajibu wao ni kuwatumikia wananchi kwa maana ya kuwahudumia wanapofika kwa ajili ya jambo fulani kwenye ofisi hizo. Kama ni ardhi, mteja anapaswa kusikilizwa shida yake na kutatuliwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu. Na kama kuna migogoro ya ardhi, maofisa wanaohusika na sekta hiyo wanatakiwa kuchukua hatua na kuitatua. 

Kutokana na dhima hiyo, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, aliwahi kusema utumishi wa umma umefanywa kichaka cha baadhi ya watu kuijinufaisha badala ya kuwahudumia wananchi. 

Ghasia alisema baadhi ya watumishi wa umma wamegeuka kuwa miungu watu kwa kuendekeza rushwa hivyo kuwafanya wananchi kuamini kwamba bila kutoa chochote kwa ofisa anayehusika kutoa huduma hiyo hawezi kuhudumiwa. Hakuishia hapo bali alisema neno ‘njoo kesho’ limekuwa msamiati maarufu katika maeneo mbalimbhali ya utumishi wa umma kwa kuwataka wananchi kurudi siku inayofuata wanapotaka huduma, sababu kubwa ikiwa kutengeneza mazingira ya rushwa. 

Hali hiyo hiyo hivi sasa imeota mizizi kuanzia ngazi ya serikali za mitaa. Mtu anapokwenda kuomba barua ya utambulisho kwa mjumbe anaombwa kutoa kati ya Sh. 2,000 na 5,000 kwa kile kinachoelezwa kuchangia gharama za viandikia. Anapofika pia ofisi ya serikali ya mtaa, anatakiwa kutoa chochote ili kupata huduma stahiki. 

Kuwapo kwa vitendo vya rushwa na miungu watu katika utumishi wa umma kumekuwa kukijidhihirisha kila mwaka wakati Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inapotoa taarifa za taasisi za umma zinazolalamikiwa kukithiri kwa vitendo vya rushwa. Miongoni mwa taasisi ambazo kila mwaka zimekuwa zikitajwa kuongoza kwa vitendo hivyo ni polisi, mahakama, serikali za mitaa, ardhi na afya. 

Juzi, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, alikutana na wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara yake na kukemea wale wanaojifanya miungu watu na kuwataka wabadilike katika utendaji wa kazi zao za kila siku. Alisisitiza kuwa jambo la kwanza katika wizara hiyo na taasisi zake ni kutoa huduma kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu na kuifanya wizara kuwa ya mfano katika utoaji huduma na kuchangia pato la taifa. 

Pamoja na kwamba Waziri Jafo amerejea kauli hiyo, jambo la watumishi wa umma kuendekeza rushwa na umangimeza huku baadhi wakijiona miungu watu na bila kutoa huduma lazima wasujudiwe na kuwapa chochote, ni la kawaida na limekuwa kama kanuni ndani ya serikali. 

Mfano halisi ni malalamiko ya wastaafu kucheleweshewa mafao yao katika mifuko ya hifadhi ya jamii. Kila wanapokwenda kufuatilia mafao yao baada ya kukoma kwa utumishi wao, wanazungushwa na kupewa kauli kuwa baadhi ya nyaraka zinakosekana, mradi watoe chochote ili wahuduniwe. Kwa ujumla jambo hili limekuwa sawa na donda ndugu  huku likionekana kukosa dawa mahsusi. 

Kama ni kusemwa, jambo hili limezungumzwa sana na viongozi wa serikali katika awamu zote tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi, hivyo kuwa sawa na ngoma iliyopigwa sana na mwisho inakaribia kupasuka.

Ni vyema sasa hatua zikachukuliwa kwa vitendo badala ya kusemwa majukwaani huku wananchi wakiendelea kuteseka na hata kutoa rushwa au kuwatumia viongozi kwa sababu ya kujuana ili kupata huduma zinazostahili. Wakati wa vitendo ni sasa ili kutokomeza rushwa, umangimeza na miungu watu katika utumishi wa umma.