Marekebisho Sheria ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto ni muhimu

Nipashe
Published at 07:13 AM Aug 30 2024
 Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis
Picha:Mtandao
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis

KUTOKANA na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinavyoendelea nchini, Bunge limeelezwa kuwa serikali inatarajia kuleta muswada wa marekebisho ya Sheria ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto.

Muswada huo una lengo la kukabiliana na vitendo vya ukatili vinavyoendelea nchini.

Suala hili limekuja wakati mwafaka kutokana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kushamiri nchini, hasa kufanyiwa vitendo vya ukatili, utekaji, mauaji na udhalilishaji.

Bunge lilielezwa kusudio hilo la Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis, wakati akijibu akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mwantumu Zodo.

Katika kipindi cha maswali na majibu mbunge huyo alitaka kujua upi mkakati wa serikali kukabiliana na vitendo vya ukatili vinavyoendelea nchini hasa kwa wanawake na watoto.

Akijibu swali hilo, Naibu waziri aliliambia Bunge kuwa muswada huo utasomwa katika mkutano huu wa Bunge kwa mara ya kwanza.

Alilifahamisha Bunge kuwa mwezi Mei, mwaka huu serikali ilizindua Mpango Kazi wa Taifa wa awamu ya pili wa Kutokomeza Vitendo vya Ukatili kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II).

Hiyo yote ni katika kuhakikisha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinatokomezwa.

Mikakati mingine iliyotajwa ni elimu kwa umma ambayo imeimarishwa kwa ushirikiano na maofisa polisi ngazi ya kata na kuanzishwa kituo cha huduma kwa wateja wizarani ili kuongeza nguvu ya elimu kwa umma na kupokea taarifa za vitendo vya ukatili.

Huduma za madawati ya jinsia na watoto zimeelezwa kuwa zinapatikana katika vituo vyote vya Jeshi la Polisi pia, idadi ya vituo vya huduma ya dharura na jumuishi kwa manusura wa ukatili imeongezeka na kufikia vituo 26 nchini.

Programu ya elimu ya malezi chanya, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto inatekelezwa kwenye mikoa na halmashauri zote nchini na kwa mwaka wa fedha 2023/24 wizara ilipata kibali cha ajira kwa maofisa Maendeleo ya Jamii 800 na maofisa ustawi 350.

Juhudi hizi za kuanzisha madawati ya jinsia na vituo vya malezi ya watoto, vinasaidia kuripotiwa kwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto ambayo hapo mwanzo yalikuwa yakiishia kwenye ngazi za familia kwa watu kuogopa kupeleka kwenye vyombo husika kwa hofu ya kutishiwa maisha au kuona fedheha.

Hali hiyo ya kuhofu ndio imesababisha baadhi ya vitendo vya ukatili kuendelea kushamiri na watoto kuteseka kwasababu ya kupata vitisho kwa wale wanao watendea vitendo hivyo.

Utafiti uliofanywa na taasisi mbalimbali umebaini kuwa ukatili dhidi ya watoto mara nyingi hufanywa na watu wa karibu wakiwamo wa ndani ya familia na walio kwenye mazingira yao ya karibu.

Sisi tunasema marekebisho ya sheria ya kuwalinda watoto dhidi ya vitendo hivyo ni muhimu na ikiwezekana hata adhabu zinazotolewa dhidi ya watu wanaofanya vitendo hivyo iongezwe ili visiendelee kufanyika na watoto waishi kwa amani.

Wazazi kwa sasa wanakuwa na hofu watoto wao wanapokuwa nje ya mazingira ya nyumbani kama watarudi salama au kufanyiwa vitendo vyovyote vya ukatili.