KATIKA kusherehekea miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika ambayo leo ni Tanzania Bara, wanawake wana mengi ya kujivunia mojawapo ni kupungua idadi ya vifo vya wazazi na watoto.
Kwa miaka mingi idadi ilikuwa kinamama 556 kwa kila vizazi hai 100,000 waliopoteza maisha.
Ni tatizo lilikuwapo kuanzia mwaka 2016 lakini juhudi zaidi zimefanyika na sasa vifo vimepungua hadi 104 mwaka huu.
Hata hivyo, wanawake wanaozaa raia wa taifa hili kuanzia wapigakura, walipakodi, wahandisi na viongozi wa kada zote wanalalamika kwanini wapoteze maisha kwenye uzazi?
Wanataka asife hata mmoja kwenye uzazi hasa kwenye changamoto ambazo zinaweza kuzuilika.
Kadhalika mafanikio mengine ambayo pia ni kupunguza vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambao nao idadi ya wanaopoteza maisha imepungua kutoka 67 kwa kila vizazi hai 1,000 hadi vifo 43 ni juhudi za kulinda uhai.
Lakini, kwani hata hao wapotee? Ni lazima juhudi zaidi zifanyike asife hata mmoja kwa sababu zinazoweza kuzuilika.
Serikali imeongeza ujenzi na kuboresha miundombinu ya huduma za afya kwa wazazi ni jambo jema linalostahili kusifiwa lakini kazi bado.
Nchi ikielekea kwenye miaka 64 ya uhuru idhibiti watoto wetu wasichana kulazimishwa kuwa mama katika umri mdogo kwa kuozwa na wanafamilia zao au kupewa mimba utotoni.
Zama hizi utaalamu upo tena wa kielektroniki wanaolaghai kuoza na kunajisi watoto hadi kupata mimba na kukatizwa masomo huku wakibebeshwa mzigo mzito wa kuwalea wamulikwe.
Ikumbuke pamoja na adha za mimba na ndoa utotoni, mwezi huu tunapoendelea na siku 16 za kuhamasisha umma kupinga ukatili wa kijinsia, tuone sote kuwa haipendezi watoto wenye miaka 14 au 13 wakiajiriwa majumbani.
Ni sheria ya kazi na mahusiano kazini ya mwaka 2004 inayoruhusu mtoto kuajiriwa ili kupata kipato.
Lakini, tujiulize ni nani anayejua hali ya mtoto huyo huko mijini anakofanyakazi?
Anatumikishwa kazi ngumu, hasomi wala hawezi kujitetea, hebu tumjali mtoto huyo kwa kukataza ajira ya watoto kwa namna yoyote ile wawe madarasani.
Sheria nyingine ambayo si rafiki wa mtoto ni ile ya ndoa ya mwaka 1971, bunge, wanaharakati, wizara na wanasheria pamoja na mahakama fuatilieni irekebishwe.
Hivi kuna haja ya watoto kuendelea kuoza wasichana au mabinti wa miaka 13 au 14 katika dunia ya sasa.
Serikali inapowezesha kupatikana huduma za kibingwa na bobezi kwa gharama nafuu kwenye hospitali za umma na kuwajali wanawake, wazazi, watoto wao isisahau kukomesha mambo yanayochangia vifo vya wazazi na watoto kwenye ujauzito ambako umri mdogo nao unahusika.
Ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo ni muhimu kuchochea kukua na uchumi afya bora, ustawi na maendeleo kwa kila mmoja.
Katika kuwa na taifa bora yote ni muhimu lakini kuandaa wanawake na watoto bora wa kizazi kijacho ni muhimu zaidi.
Hawa wataandaliwa kwa kuboresha sekta zote mtambuka kuanzia ya afya, elimu, teknolojia, kilimo ili kupata chakula, usalama, sheria na ulinzi.
Ni kazi njema ya kusambaza dawa, vifaa tiba na chanjo kwa watoto, lakini kama hawatalindwa dhidi ya unyanyasaji kingono, utoro shuleni, udumavu, utumikishwaji majumbani, dhuluma za kuozwa utotoni, kukeketwa itakuwa ngumu kuwa na vizazi vya sasa vilivyolindwa ili kupata Tanzania bora ya kesho.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED