EWURA yahamasisha uvunaji wa maji ya mvua, matumizi ya nishati safi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:56 PM Dec 13 2024
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeendesha mafunzo kwa wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) jijini Dar es Salaam, ikilenga kuimarisha uelewa wa wanahabari kuhusu sekta za nishati na maji.

Mafunzo hayo yameendeshwa leo Desemba 13,2024 yameweka msisitizo maalum kwenye uvunaji wa maji ya mvua kama mbinu ya kukabiliana na changamoto za upungufu wa maji katika maeneo mbalimbali, pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia na kwenye magari.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk. James Andilile, amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea wanahabari uwezo wa kuripoti taarifa za sekta ya nishati na maji kwa usahihi, hatua inayolenga kuchochea maendeleo ya taifa.

“Wanahabari wanajukumu kubwa la kutoa taarifa sahihi na kwa wakati. Tunawawezesha kuelewa zaidi kuhusu uvunaji wa maji ya mvua na umuhimu wa matumizi ya nishati safi, mambo ambayo yana mchango mkubwa katika maendeleo endelevu,” amesema Kaguo.

Mafunzo hayo pia yalihusisha historia ya EWURA, majukumu yake ya udhibiti katika sekta za umeme, petroli, gesi asilia, na maji, pamoja na mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006.

Katibu wa JOWUTA, Suleiman Msuya, alishukuru EWURA kwa mafunzo hayo na kuwataka wanahabari kutumia elimu waliyoipata kuboresha taarifa zinazohusu sekta ya nishati na maji.

“Mafunzo haya yameongeza maarifa yetu, na sasa tutaweza kuelimisha umma kwa usahihi zaidi kuhusu masuala ya nishati na maji,” amesema Msuya.

Mafunzo haya yamekuja wakati mwafaka, yakitarajiwa kusaidia kuhamasisha matumizi endelevu ya maji na nishati nchini Tanzania.