RAIS mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mbio za ‘Rombo Marathon 2024’ zitakazofanyika Disemba 23 katika eneo lenye miinuko, msitu wa asili na ile inayomilikiwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) ya Rongai Forest yenye kivutio maalum cha nyani wa aina nne.
Mbio hizo zitakazowahusisha zaidi ya wakimbiaji 1,200, pia zinatazamiwa kuwavutia watu mbalimbali kati ya 3,000 mpaka 5,000 walioingia mkoani Kilimanjaro ‘kuhiji’ sikukuu za mwisho wa mwaka za Krismasi na mwaka mpya.
Akizungumzia maandalizi ya mbio hizo leo Desemba 13, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala, amesema Kikwete (JK), ataambatana na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolph Mkenda, ambaye pia ni Mbunge wa Rombo.
“Ndugu zangu, unapokuja Rombo Marathon, ndiyo sehemu pekee za kubwaga stress zako (msongo wa mawazo), kwa sababu utakutana na misitu ya asili, misitu yenyewe imezungukwa na nyani zaidi ya aina nne.
“Utakuwa unakimbia huku unapata utalii, wakati huo huo unapata hewa ile ya asili kabisa. Kwa nini uje Rombo Marathon, ukija Rombo Marathon, siyo kukimbia tu, baada ya kukimbia tuna ‘Ndafu Festival’
…Ambayo pale utapata kwanza vyakula vya asili ya Kichaga, utaikuta ngararumo, utakuta mtori, utakuta kitawa, utakuta machalari, lakini utakutana na vyakula vingine vyote vya asili ya kichaga. Siyo hivyo tu utakutana na kinywaji maarufu sana an ni maalum kwa ajili ya Wachaga, nacho kinaitwa mbege.
Zaidi ameongeza, “Njooni Rombo Marathon, mkija Rombo Marathon hamtajutia, ni sehemu pekee ambayo utaenda kumaliza mwaka wako vizuri, utaumaliza ukiwa na amani, utaumaliza ukiwa na furaha, utaumaliza ukiwa na network iliyo contain nchi nzima. Changia shilingi 40,000 ili uweze kupata burudani.”
Mratibu wa mashindano hayo ya Rombo Marathon, Themistockles Isdory, ameeleza kuwa kutakuwa na mbio zinazohusisha kilomita 21 (Half Marathon), mbio za kilomita 10, ambayo ni mikimbio ya msituni inayofahamika kama ‘Trail’ na vilevile yatakuwa na mbio za kilomita tano, ambayo na yenyewe ni ya msituni.
Hapa Themistockles anaeleza zaidi, “Mbio hiyo ya kilomita tano, ni ya social runners, nikiwa namaanisha ni mtoko wa kifamilia. Watoto kuanzia miaka mitano, wakiwa na wazazi wao na walezi wao na mama zao, wanaruhusiwa kushiriki. Lakini watu wazima, ambao umri umeenda na wale wenye unene wanaruhusiwa kushiriki mbio za kilomita tano.”
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED