KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mbunge mstaafu wa Mpanda Mjini, Said Amour Alfi, amesema ni makosa makubwa kushabikia kukandamizwa kwa vyama vya upinzani katika uchaguzi mbalimbali nchini.
Amesema kuwapo kwa wawakilishi wake katika nyadhifa mbalimbali ni chachu ya kuchagiza maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Kada huyo ambaye aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara na mbunge wa Mpanda kwa miaka 10 kupitia chama hicho kabla ya kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) alisema hayo juzi alipozungumza na waandishi wa Habari nyumbani kwake, mjini hapa.
"Sisi Chama Cha Mapinduzi tutafanya makosa makubwa sana kama tutatumia rasilimali zetu na nguvu zetu na maarifa yetu kuua upinzani. Lazima tuache upinzani ukue kwa kuwa una faida nyingi sana katika ustawi wa taifa hili,” alisema.
Alitolea mfano wakati wa utawala wa awamu ya nne, ambapo mikoa ya kanda magharibi kwa maana ya Rukwa, Katavi, Tabora na Kigoma ilikuwa haijafunguka kimiundombinu, hivyo kutofikika kiurahisi, lakini nguvu ya vyama vya upinzani ilisaidia Serikali kuifungua mikoa hiyo.
Alisisitiza kua upinzani ni kichocheo cha maendeleo na ni fursa kwa upande wa pili kuieleza na kuikosoa serikali kuhusu kasoro zilizopo na hatua stahiki zinazopaswa kuchukuliwa.
Kwa mujibu wa Arfi, awamu ya tano ndiyo iliyojielekeza kuumaliza upinzani na ilifaulu kufanya hivyo, hali ambayo ilisababisha kutokuwapo watu au wanasiasa wanaokosoa serikali, kitu ambacho ni hatari kwa ustawi wa maendeleo ya taifa.
"Niwaeleze wana CCM wenzangu, tutakuwa tunajidanganya kama tutaamini kwamba tumeua upinzani. Kiuhalisia upinzani hauonekani ila upo katika mioyo ya watu, hivyo tusijidanyanye," alisema.
Kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, alisema kwa maoni yake hakufurahishwa na mchakato mzima ikiwa ni pamoja na matokeo yake.
Alisema watendaji wa walifanya mambo ambayo hawakuagizwa na CCM, bali kwa matakwa yao binafsi tu wakawakandamiza wapinzani.
"CCM isiwe sababu ya kukandamiza demokrasia. Tutoe haki kwa hivi vyama na isivyo bahati sana, CCM wakati mwingine inahusishwa katika haya mambo ni kutokuwa na uaminifu na dhamira njema ya kutazama hii nchi kama ni nchi yetu sote.
“Viongozi wanaosimamia uchaguzi ndio chanzo cha mifarakano yote, na wao ndio wanaruhusu kura feki kuingia katika masanduku, wasiokuwa na haki wanapiga kura. Tuwaeleze watendaji wetu watende haki. Bila kuwapo haki tutaliua hili taifa na si vinginevyo," alisema.
Arfi alishauri kuwa kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi huo zisijirudie ili Uchaguzi Mkuu ujao uwe huru na haki na kuondoa malalamiko yasiyo na tija kwa wananchi na vyama vya siasa vya upinzani.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, alitangaza matokeo ya jumla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27 mwaka huu, akisema kuwa CCM ilipata ushindi wa jumla wa wenyeviti wa serikali za vijiji kwa nafasi ya viti 12,150 sawa na asilimia 99.01.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED