UNFPA, Japani wakabidhi gari, vifaa tiba Kigoma

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 05:04 PM Dec 13 2024
Balozi wa Japan nchini Yasushi Misawa kulia Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa na Mwakilishi Mkazi wa UNFPA Mark Bryan Schreiber wakati wa makabidhiano ya gari.
Picha:Mpigapicha Wetu
Balozi wa Japan nchini Yasushi Misawa kulia Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa na Mwakilishi Mkazi wa UNFPA Mark Bryan Schreiber wakati wa makabidhiano ya gari.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) Tanzania, kwa kushirikiana na Serikali ya Japani, limekabidhi gari na vifaa tiba kwa uongozi wa Mkoa wa Kigoma.

Msaada huo ulikabidhiwa kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa, katika hafla iliyofanyika nyumbani kwa Balozi wa Japan nchini, Yasushi Misawa, jijini Dar es Salaam jana, ikihudhuriwa na wadau mbalimbali wa afya.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Balozi Misawa alisema msaada huo ni sehemu ya mradi wa bajeti ya ziada ya Japani wenye thamani ya Dola za Kimarekani 359,964 uliotolewa kupitia UNFPA kwa kipindi cha mwaka mzima.

"Ubalozi wa Japani umetekeleza miradi mbalimbali, ikiwemo ya elimu ya afya na usafi wa mazingira katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Kigoma kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita," alisema Balozi Misawa.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa UNFPA Tanzania, Mark Bryan Schreiner, alisema ushirikiano huo unadhihirisha mikakati ya pamoja ya kuhakikisha hakuna mwanamke au msichana anayeachwa nyuma.

"Tunaamini msaada huu kutoka Serikali ya Japani utasaidia kuendeleza na kupanua huduma muhimu za afya zinazookoa maisha, hivyo kuiwezesha jamii kwa ujumla," alisema Schreiner.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Thobias Andengenye, aliushukuru Ubalozi wa Japani na UNFPA kwa msaada huo.

"Msaada huu sio tu utaimarisha mfumo wa afya mkoani Kigoma, bali pia utaokoa maisha kwa kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata huduma wanazohitaji kwa haraka," alisema Rugwa.