Lissu afunguka mazito kumvaa Mbowe

By Restuta James , Nipashe
Published at 10:04 AM Dec 13 2024
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, akisalimiana na wanachama wa chama hicho, baada ya kuzungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amepandisha joto ndani ya chama hicho baada ya kutangaza kugombea uenyekiti wa wa taifa huku akisimamia ajenda saba.

Kwa kutangaza huko, Lissu atamvaa Mwenyekiti wa CHADEMA aliyeko madarakani, Freeman Mbowe.  Lissu alitangaza azma hiyo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, ambao pia ulihudhuriwa na wawakilishi wa kanda nane za CHADEMA, akiwa na kaulimbiu ya ‘Nuru Mpya, Mwelekeo Mpya, Mapambano Mpya.’

Lissu alisema ikiwa atashindwa kwa haki kwenye uchaguzi huo, atabaki kuwa mwanamageuzi na atakubali matokeo na kusisitiza kwamba hayuko tayari kuharibu chama alichokijenga kwa jasho na damu kwa  miaka 20.

“Nikishindwa kwenye uchaguzi huru na haki sitakuwa na cha kusema. Kukiwa na mambo ya kihuni, kuna mtu ataniambia nisilie, ninyamaze, sitanyamaza,” alisema huku akisisitiza hana mgogoro na Mbowe japokuwa wamekuwa wakitofautiana kwenye baadhi ya mambo.

Alitoa mfano kwamba hakukubaliana naye kwenye suala la maridhiano na CCM na kwamba anaamini ulikuwa msimamo sahihi.

AGENDA ZAKE SABA

Alisema agenda yake ya kwanza ni kufanya siasa katika kile alichoita mazingira mapya, ambayo yalianza baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Alisema tangu mwaka 2015, Tanzania iliingia kwenye utawala usiokubali ushindani kupitia uchaguzi huru na haki.

Lissu ambaye ni mwanasheria kitaaluma, alisema nchi iko kwenye kipindi cha siasa za kidhalimu, zinazotumia vyombo vya dola kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kushinda uchaguzi.

Aina hiyo ya siasa, alisema  imefanikisha CCM kuongoza mitaa, vijiji na vitongoji vyote mwaka 2019, wabunge na madiwani wengi kutokana na CCM kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2020 na kushinda kwa kishindo uchaguzi wa mwezi uliopita.

Kwenye uchaguzi uliofanyika mwezi uliopita, alisema wagombea wengi wa upinzani walienguliwa kwa madai ya kukosa sifa kama ilivyofanyika mwaka 2019.

Lissu alisema ili kushindana kwenye hali ya sasa, CHADEMA inahitaji kuendelea kudai Katiba Mpya ya Kidemokrasia, Mfumo Mpya wa Uchaguzi wenye Tume Huru, Sheria Bora ya Uchaguzi na haki kwa watu wote.

Kwa mujibu wa Lissu, agenda yake ya pili ni kuisuka upya katiba ya CHADEMA ili kuweka ukomo wa madaraka ya uongozi ndani ya chama hicho na kwa wabunge na madiwani wa viti maalum.

“Pia kuweka ukomo wa madaraka katika uongozi wa chama si tu utaondoa uwezekano wa viongozi kung’ang’ania madaraka, bali utawezesha kujengeka kwa utamaduni wa kuandaa viongozi wapya wa chama wa kila kizazi.

“Ukomo wa madaraka utapunguza sana, kama si kuondoa kabisa, upambe na uchawa unaoshamiri pale viongozi wanapong’ang’ania madaraka katika mazingira yasiyokuwa na ukomo wa Madaraka,” alisema. 

Kuhusu ukomo katika nafasi za viti maalum, alisema zitawawezesha wanawake kupata uzoefu na uwezo wa kisiasa na kiuchumi katika shughuli za bunge na halmashauri za serikali za mitaa.

Lissu alitaja agenda nyingine kuwa ni kuweka mfumo wa uchaguzi ndani ya chama, ambao utaundwa ndani ya Katiba ya chama hicho.

Alisema lengo ni kupata viongozi waadilifu na wanaoweza kuendesha siasa katika mazingira ya sasa na kuweka mkazo wa kuheshimu taratibu za uchaguzi katika ngazi zote, ili kuondoa mipasuko.

“Kuacha kuzingatia na kuheshimu Katiba ya chama ni kukaribisha kila aina ya uhuni, rushwa, uonevu na mambo ya hovyo katika uendeshaji wa chaguzi za chama chetu.

“Kama ambavyo tunahitaji Tume Huru ya Uchaguzi na mfumo huru wa uchaguzi katika chaguzi zetu za umma, ndivyo tunavyohitaji chombo huru cha kusimamia chaguzi zetu za ndani ya chama,” alisema.

Alisema lengo ni kuwahakikishia wagombea wa nafasi mbalimbali kuwa watatendewa haki na wasimamizi wa uchaguzi katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi.

“Haya yote yanawezekana endapo tutarekebisha Katiba yetu ya chama ili kuweka mfumo huru wa kusimamia chaguzi za chama,” alisema.

Agenda nyingine ni kuweka utaratibu mpya wa kutafuta, kusimamia na kutumia fedha na rasilimali za chama hicho. Alisema utaratibu wa sasa umeweka utegemezi kwa watu wachache ndani ya chama kutafuta fedha na rasilimali za chama.

KWA NINI LISSU?

Alisema amejipima na kuona anafaa kuongoza chama hicho ngazi ya taifa kwa kuwa ana historia ya uadilifu na kukubalika na jamii.

“Napenda kuamini kwamba historia ya uadilifu wangu na kukubali kwangu na jamii ya Watanzania inajulikana wazi na Watanzania walio wengi. Hatua hii ya mapambano inahitaji kiongozi aliyeonyesha kwa tabia, mwenendo wa uzalendo wa kupenda na kutetea nchi yake na msimamo wa kuaminika.

“Uzalendo wangu na msimamo wangu umepimwa na kuthibitishwa katika mapito na majaribu mengi ambayo nimepitishwa takribani miongo mitatu ya maisha yangu ya utetezi wa haki za wananchi wetu, na rasilimali za nchi yetu. Kwa sababu hizo, ninaamini nina sifa hizo mahsusi na nyingine zilizotajwa katika Katiba yetu ya chama.

“Uzoefu wangu wa kitaaluma na kisiasa; kwa historia yangu ya utumishi katika chama, bungeni na kwingineko, na kwa msimamo wangu thabiti na usiotetereka, ninazo sifa na uwezo wa kusimamia maboresho yote yanayohitajika katika uendeshaji bora wa shughuli za chama chetu katika kipindi hiki kigumu,” alisema.