ZAIDI ya nyumba 15 zenye wakazi zaidi ya 30 katika Kijiji cha Moya Mayoka, kata ya Magara, wilayani Babati, mkoani Manyara, zimezingirwa na mawe na tope lililoshuka kutoka Mlima Magara na kusababisha wananchi kukimbia tope.
Akizungumza na Nipashe jana kwa njia ya simu, Diwani wa Kata ya Magara, Jacob Bilikuli alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 1:00 asubuhi.
"Eneo ambalo mawe na tope vimeshuka mpaka kwenye makazi ya wananchi ni zaidi ya ekari 10 ambapo mawe na tope vimeharibu nyumba za wananchi," alisema Bilikuli.
Aidha, alisema athari zingine zilizopatikana ni mifugo na vyakula kusombwa na maji na kufunikwa tope na mawe.
Alisema baada ya kutokea maafa hayo waliwahamisha wananchi waliopoteza makazi na kuwahifadhi Shule ya Msingi Moya Mayoka.
Pia, alisema wanaendelea kumsubiri Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda ili washauriane cha kufanya.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Magara, Hawa Nyoni akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Manyara, Lucas Mwakatundu, alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu tukio hilo, alisema hajapata taarifa na kuahidi kufuatilia ili kujua ukweli wa tukio hilo.
Kijiji cha Moya Mayoka kinapakana na Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED