Makinda aandika rekodi mpya miaka 10 ya MoCU

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 07:20 PM Dec 13 2024
Anne Makinda, Mkuu wa Chuo Kikuu MoCU, akimtunuku mmoja wa wanazuoni.
Picha: Mpigapicha Wetu
Anne Makinda, Mkuu wa Chuo Kikuu MoCU, akimtunuku mmoja wa wanazuoni.

SPIKA zamani wa Bunge, Anne Makinda, amewatunuku kwa mara ya kwanza Shahada ya Udaktari wa Falsafa (PhD) ya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, wanazuoni sita waliofuzu vigezo vya kitaaluma katika fani mbalimbali za ubobezi, tangu Rais Samia Suluhu Hassan, amteue kuwa Mkuu wa Chuo hicho mwezi Agosti mwaka 2023.

Makinda, ambaye ni Mkuu wa Chuo hicho cha Ushirika Moshi (MoCU), ndiye Spika wa kwanza mwanamke katika Bunge la Tanzania.

Kabla ya kutunuku shahada hizo jana katika mahafali ya 10, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, George Yambesi, alimweleza Makinda kuwa kati ya wahitimu 3,246 atakaowatunuku astashahada, stashahada, shahada za awali, stashada za uzamili na shahada za umahiri, wamo wanazuoni sita waliofuzu kupewa shahada ya uzamivu.

Wanazuoni hao, ni Dk. Alex Nyagango, aliyefanya utafiti juu ya matumizi ya simu za mkononi katika kuwawezesha wakulima wa zabibu kupata taarifa za masoko mkoani Dodoma, Tanzania.

Mwingine ni Mtawa wa Kanisa Katoliki Tanzania, Dk. Bernadette Temba, aliyefanya utafiti juu ya ufanisi wa biashara zinazoendeshwa na Kanisa Katoliki na zile zisizo za kanisa; utafiti linganishi kwa miradi ya Kanisa Katoliki na Miradi ya Ufugaji Kuku ya Kibo Poultry Tanzania.

1

Aidha, yumo Dk. Emmanuel Mkilia, aliyefanya utafiti juu ya athari za kiusalama kwa mtandao wa matumizi ya huduma kibenki mtandaoni nchini Tanzania.

Pia, Makinda, amemtunuku Shahada hiyo ya Udaktari wa Falsafa, Dk. George Budotela, ambaye amefanya utafiti wa vizuizi vya mikopo isiyolipika miongoni mwa Benki za Biashara nchini Tanzania.

 Vilevile, Dk. Julieth Koshuma, aliyefanya utafiti kuhusu mpango wa matumizi ya kilimo mkataba chini ya muundo wa ushirika na utendaji wa wakulima wadogo katika Bonde la Kilombero, Mkoa wa Morogoro, ametunukiwa shahada hiyo na Makinda.

Mwanazuoni mwingine, ni Pamela Liana, aliyefanya utafiti unahusu kutoa fedha kwa njia ya simu kwenda malipo kwa njia ya simu, kupima tabia za watumiaji katika uzoefu wa kidijitali nchini Tanzania.

Awali, Makamu Mkuu wa Chuo hicho cha MoCU, Prof. Alfred Sife, alimweleza Spika mstaafu Makinda, wanazuoni hao na wahitimu wengine, ni alama tosha ya mafanikio ya kujivunia katika maisha yao, kwani inatokana na juhudi na maarifa waliyowekeza.