MKOA wa Tanga unakabiliwa na tatizo la vijana wapatao 30,000 ambao hawataki kutafuta kazi na kusoma na kuwa mzigo katika jamii.
Takwimu hizo zimo katika hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilida Buriani iliyosomwa wakati wa Uzinduzi wa Jukwaa la Vijana Wilaya ya Tanga uliofanyika jana katika Viwanya vya Shule ya Kimataifa ya Tanga.
Balozi Batilda, alisema katika Jiji la Tanga, tatizo la ajira kwa vijana ni changamoto inayolikabili, hivyo hawana budi kupambana nayo kwa nguvu zote kwa kushirikisha Serikali na wadau wengine wa maendeleo.
Alisema kulingana na sensa ya Taaisis ya Takwimu ya Taifa (NBS), bado changamoto ya ajira kwa vijana ni kubwa na kila mmoja anahitajika kuchukua hatua wakiwemo vijana wenyewe kwa kutafuta ajira na kujiajiri.
Alisema takwimu hizo za NBS, zinaonyesha kuwa vijana 147,000 wenye umri wa miaka 15-35 katika jiji hilo 109,000 wameajiriwa katika sekta rasmi na isiyo rasmi,
“ Lakini wapo takriban 5,000 wanatafuta kazi kwa sasa. Inasikitisha sana kuona kuwa kuna vijana takriban 30,000 hawatafuti kazi na wala hawataki kusoma. Hili ni tatizo la kijamii na nilazima tushirikiane kulitatua,” alisema
Alisema Serikali inatambua changamoto hiyo ya ajira kwa vijana na kuchukua hatua ya kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wa ndani na nje nchi kuendeleza kundi hilo.
Vilevile, alisema serikali imefanya mapitio ya sera a vijana na kutengeneza nyingine kusaidia upatikanaji wa ajira na kujiajiri kwa kundi hilo.
“ Jiji la Tanga limekuwa mstari wa mbele kuhakikisha vijana wanatumia fursa zilizoko kujiajiri na kuajiriwa kwa kuweka mazingira mazuri ya wadau kufanya kazi,” alisema.
Batilda, alitoa mfano katika awamu ya kwanza ya mradi wa TangaYetu, miradi mbalimbali katika sekta za uzalishaji mali ilitekelezwa na kunufaisha vijana.
Alitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni wa utengenezaji na ugavi wa madawati kwa shule za msingi na sekondari.
Alisema mradi huo umetoa ajira za muda mfupi kwa vijana 123, kati yao 10 ni wenye ulemavu.
Aliutaja mradi mwingine kuwa ni kubadili fikra na ujasiriamali kwa vijana kwa kunufaisha 1,036 na kjuanzisha vikundi 17 vya kuweka na kukopa kwa kuwawezesha vijana kukopeshana, kuanzisha na kuendeleza biashara zao.
“Mpaka kufikia mwisho wa mradi, vikundi hivyo vilikuwa vimeweka kiasi cha shilingi milioni 13,” alisema .
Alisema vilevile, Mradi wa Fursa za ajira kwa vijana kwa njia ya mtandao; uliwafikia vijana 100 na kuwapatia mafunzo ya jinsi ya kutambua fursa za mitandaoni na namna ya kutumia simu janja kujipatia kipato.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, zaidi ya vijana 45 waliofanikiwa kumaliza mafunzo na kupata kazi za muda mfupi katika kampuni ya simu nchini.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED