Amref Tanzania yakabidhi magari TAMISEMI, kuimarisha huduma za afya Mara,Simiyu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:58 PM Dec 12 2024
 Amref Tanzania yakabidhi magari TAMISEMI, kuimarisha huduma za afya Mara,Simiyu
Picha: Mpigapicha Wetu
Amref Tanzania yakabidhi magari TAMISEMI, kuimarisha huduma za afya Mara,Simiyu

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya afya, Dk. Grace Magembe, ametoa wito kwa Makatibu Tawala wa Mikoa ya Mara na Simiyu kuhakikisha magari wanayokabidhiwa yanatunzwa vyema ili yaweze kuendelea kutoa huduma za afya kwa muda mrefu zaidi.

Dk. Grace alitoa maelekezo hayo jana tarehe 11 Desemba 2024, katika hafla ya kukabidhi magari mawili kwa Makatibu Tawala wa mikoa hiyo, walioakilishwa na Waganga Wakuu wa Mikoa, katika viwanja vya Ofisi za TAMISEMI jijini Dodoma. Magari hayo yametolewa na Taasisi ya Amref Health Africa Tanzania kwa lengo la kuimarisha usimamizi shirikishi wa shughuli za afya katika mikoa hiyo.

"Magari haya yanapokabidhiwa kwetu, tuna wajibu wa kuendelea kuyatunza na kuhakikisha yanafanya kazi vizuri ili kuwahudumia wananchi," alisema Dk. Grace.

Aidha, Dk. Grace alitumia fursa hiyo kuipongeza Taasisi ya Amref Health Africa Tanzania pamoja na wadau wengine kwa ushirikiano wao mzuri na Serikali katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi. Alisisitiza kuwa ushirikiano huo umeleta mafanikio makubwa katika sekta ya afya, hususan maeneo ya vijijini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Amref Health Africa Tanzania, Dk. Florence Temu, alibainisha kuwa taasisi hiyo imekabidhi jumla ya magari sita kwa mikoa ya Mara na Simiyu, ambapo kila mkoa umepewa magari matatu.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa sekta ya afya, ambao walisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kuhakikisha rasilimali zinazotolewa na wadau zinatumika kwa manufaa ya wananchi.