MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Februari 26, mwakani, inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya mauaji inayomkabili mfanyabiashara Khamis Luwonga (38), anayeshtakiwa kumuua mkewe Naomi Marijani na kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa.
Vilevile, mahakama hiyo imeongeza siku 14 kwa upande wa Jamhuri kufanya majumuisho ya mwisho katika kesi hiyo na kuyawasilisha mahakamani Desemba 24, mwaka huu huku mshtakiwa akiwa tayari ameshawasilisha majumuisho hayo.
Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa na Jaji Hamidu Mwanga baada ya kusikiliza mashahidi 14 wa upande wa mashtaka na utetezi. Mahakama pia ilipokea vielelezo mbalimbali, ukiwamo udongo wenye masalia ya mafuta yanayodhaniwa kuwa ni ya mwili wa Naomi.
Wakili wa Serikali Cuthbert Mbilingi alidai jana mbele Jaji Mwanga kwamba hawakufanikiwa kuwasilisha majumuisho ya mwisho kama ilivyoelekezwa na mahakama kwa sababu kompyuta aliyokuwa anatumia ilipata hitilafu.
"Tunaomba tuongezwe muda wa nyongeza hadi Desemba 24, 2024 tutakuwa tushayawasilisha mahakamani," alidai Wakili Mbilingi.
Wakili wa Mshtakiwa, Hilda Mushi alidai wao waliwasilisha majumuisho hayo Desemba 10, mwaka huu, kama walivyopewa amri na mahakama.
"Tumepewa muda wa siku 14, lakini wao hawajafanya hivyo na hakuna sababu ya msingi waliyotoa, walichokizungumza hakina mashiko, hata hajasema hilo tukio lilitokea lini.
"Tunataka haki iweze kutendeka kwa sababu mteja wangu ameshakaa muda mrefu gerezani, anatakiwa apate haki, sisi tunaomba tarehe ya hukumu," alidai Wakili Hilda.
Wakili Mbilingi alidai kuwa siku mbili kabla ya kuwasilisha majumuisho, ndipo hitilafu hiyo ilitokea, hivyo ili haki itendeke wanaomba wapewe nafasi ya kuwasilisha.
"Tumkubalie kwa sababu ni msaada wa mahakama katika kufikia haki, tuwakubalie tu kwa sababu tunakwenda likizo na sababu uamuzi utatolewa mwakani," Jaji Mwanga alisema.
Jaji huyo alitoa siku 14 kwa upande wa Jamhuri kuwasilisha majumuisho hayo hadi Desemba 24, mwaka huu wawe wameshafaili na hukumu itasomwa Februari 26 mwakani.
Hata hivyo, mshtakiwa alinyoosha kidole na alipopewa nafasi, akaanza kuulalamikia upande wa Jamhuri kushindwa kuwasilisha mahakamani majumuisho hayo ndani ya siku 14.
"Wala usiwe na wasiwasi, huu hata si ushahidi, ni uchambuzi tu ambao na uhalisia wa hii kesi mahakama inahitaji haya wala usiwe na presha kwa sababu unaweza hata ukakusaidia na wewe pia," alisema Jaji Mwanga.
Katika kesi hiyo ya mauaji namba nne ya mwaka 2019, mshtakiwa Luwonga ambaye ni mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam, anadaiwa Mei 15, 2019, akiwa Gezaulole, Kigamboni alimuua Naomi Marijani.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED