Mbowe, Lissu wazua jambo mitandaoni

By Restuta James , Nipashe
Published at 09:51 AM Dec 12 2024
Mbowe, Lissu wazua jambo mitandaoni
Picha:Mtandao
Mbowe, Lissu wazua jambo mitandaoni

KITENDO cha Mwenyekiti Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe kuonekana hadharani akiwa na Makamu wake, Tundu Lissu, kumeibua shangwe mitandaoni, huku baadhi ya wafuasi wa chama hicho wakiendelea kunyukana.

Nipashe imefuatilia maoni kwenye kurasa za chama hicho na ya makada wenye ushawishi mtandaoni, yakionesha mivutano; baadhi wakitaka Mbowe ang’atuke ili ampishe Lissu, wengine wakimtaka Lissu aache wanachodai "kukivuruga chama". 

Baada ya kuwapo tetesi kwamba wawili hao hawaelewani kutokana na kinachodaiwa "mpango wa Lissu kuwania nafasi ya uenyekiti wa CHADEMA katika uchaguzi wa ndani ya chama, juzi Mbowe na Lissu walijitokeza wakiwa pamoja mbele ya waandishi wa habari na kuzungumzia hadharani suala hilo. 

Vilevile, barua ya kumhoji Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Iringa Mjini, Frank Nyalusi, kuhusu sababu za kuwaondoa mawakala katika vituo siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita, umeongeza mnyukano miongoni mwa makada hao mitandaoni. 

Aliyekuwa mgombea wa CHADEMA katika Jimbo la Mbarali, mkoani Mbeya, Liberatus Mwang'ombe, amekosoa barua ya kuhoji uamuzi wa Nyalusi, akiihusisha na msimamo wake wa kumuunga mkono Lissu. 

Mwang’ombe alisema kwenye mtandao wa X juzi, kwamba uamuzi wa Nyalusi kuondoa mawakala Novemba 27, ulitokana na wengi wao kuzuiwa kuingia katika vyumba vya kupigia kura kwa madai ya barua zao kukosa mhuri wa moto na waliruhusiwa kuingia vituoni baadaye saa sita mchana. 

Barua kwa Nyalusi iliyoandikwa na Baraza la Uongozi Mkoa wa Iringa na kutiwa saini na Katibu wake, Leonard Kurwawijilla, imemtaka ajieleze kwa kuwaondoa mawakala vituoni, kukaidi maagizo ya viongozi wa CHADEMA Iringa na Kanda, kuanzia Katibu, Mwenyekiti wa Mkoa na Mwenyekiti wa Kanda, la kumtaka awarudishe na kuwatangazia wanachama wa chama hicho Jimbo la Iringa wasiende kupiga kura. 

Barua hiyo ambayo imewekwa kwenye mitandao ya kijamii, ilieleza kuwa uamuzi wa Nyalusi umekinyima chama hicho nafasi ya kutokujua dosari za uchaguzi huo na hivyo kukinyima uhalali wa kuukosoa, jambo ambalo ni utovu wa nidhamu. 

Nyalusi ametakiwa kujieleza ndani ya siku 14 kuanzia Jumatatu ya juma hili alipopewa barua hiyo. 

Mwang’ombe alidai kuwa barua hiyo imetokana na uamuzi wake wa kuonesha kumuunga mkono Lissu, kwa kuwa kikao cha tathmini ya uchaguzi Iringa kilikaa Novemba 28, 2024 na kuhoji sababu za barua ya kilichoamuliwa kuandikwa wiki mbili baadaye. 

Maoni mengi ya makada na wafuasi wa CHADEMA, yalimkosoa Mwang’ombe huku wengine wakimtaka Nyalusi ajibu barua badala ya kulalamika mtandaoni. 

Kada wa CHADEMA, Yeriko Nyerere, aliandika kwenye ukurasa wake wa X kwamba wanachama wa chama hicho wanasubiri kuingia katika uchaguzi ngazi ya taifa, lakini hawatamuunga mkono mgombea "anayekishambulia" chama hicho hadharani na sirini. 

"Sisi kama wanachama, yeyote anayetafuta uongozi kwa kuungwa mkono na maadui zetu, CCM, huyo siyo mwenzetu, yeyote anayetafuta uongozi kwa kushambulia viongozi wenzake, huyo siyo mwenzetu! Yeyote anayegeuza mkuki kwetu huyo ni adui!  

"Tutapambana naye sawasawa na tunavyoshughulika na ma-CCM, haijalishi ni kiongozi wa kitaifa ama ana heshima gani katika taifa. 

"Hatuna chama kingine mbadala nchini, hiki chama lazima tukilinde kwa wivu mkubwa, dola iko kazini kuhakikisha chama kinaanguka na kufutika, uzembe wetu kidogo tu utakigharimu chama chetu! Chama kwanza mtu baadaye," aliandika. 

Kada mwingine Martin Maranja, aliposti picha ya Mbowe na Lissu wakiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari juzi, ambayo ndani ya saa mbili ilikuwa imetazamwa na watu 13,000 huku ikipata maoni 731. 

Baadhi ya watu waliotoa maoni kwenye picha hiyo, waliwakosoa waliokuwa wanasema "CHADEMA ina mpasuko". 

"Kuna wachawi humu kutwa kusema Mbowe na Lissu hawapatani, sasa hii ni nini?” walihoji wachangiaji wengi kwenye mtandao wa X juzi. 

Juzi kwenye mkutano na waandishi wa habari, Mbowe aliwajibu wanaomtaka ang’atuke kwenye nafasi ya uenyekiti na kusema watakaomwambia aondoke ni wanachama na watakaomwambia agombee ni wanachama. 

"Mimi ninashangaa tu huko mitandaoni, pilipili usiyoila inakuwashia nini?" Mbowe alihoji. 

Lissu alisema haogopi maneno ya mtandaoni kwa kuwa anaishi na risasi mwilini, hivyo hana anachoogopa. 

Mara kadhaa, Lissu amekaririwa akidai "kumepenyezwa fedha chafu ndani ya CHADEMA" na ndio maana amekuwa akikema rushwa hadharani. 

Mwezi uliopita, Mbowe alisema tofauti ya mitazamo kati yake na Lissu, haina maana kuwapo mpasuko wala ugomvi ndani ya CHADEMA, bali ni uimara wa chama. 

"Hatuna ugomvi, hayo ni mambo ya kawaida tu. Ukishakuwa na chama cha siasa kisichokuwa na minyukano, hicho chama ni mfu. Siasa ndivyo ilivyo. Mkiwa kwenye siasa mnakubaliana kila kitu kwa asilimia 100 siku zote, hiyo safari hamtoboi," alisema Mbowe Novemba 19 mwaka huu kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Leo Lissu anatarajiwa kuzungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Ajenda yake haijawekwa wazi.