VYAMA vya upinzani nchini vimesema kunahitajika nguvu ya pamoja ya wadau wa siasa kupigania Katiba mpya na maboresho katika mifumo ya uchaguzi ili kuwa na uchaguzi huru na wa haki na kuepuka yaliyotokea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Ni rai iliyotolewa juzi wakati wa mdahalo ulioandaliwa na Mtandao wa Jamii Forums kwa ajili ya tathmini ya Uchaguzi wa Serikali ya Mitaa, ukiangazia ukiukwaji wa sheria za uchaguzi na mambo ya kujifunza.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), John Pambalu alisema ili kurekebisha yaliyotokea katika uchaguzi huo, viongozi wa vyama vya upinzani, wanazuoni, viongozi wa dini, watu mashuhuri na makundi mbalimbali wanapaswa kuungana na kupigania mabadiliko ya Katiba yatakayoleta uchaguzi huru na wa haki.
Alisema nchi inapojiandaa kwa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Novemba mwakani kunahitajika nguvu ya umma kuibana serikali, ili kuwapo Katiba mpya au kufanya maboresho madogo katika mifumo ya uchaguzi, hivyo kushughulikia mambo yote yanayohusiana na uchaguzi kikatiba na si kikanuni.
"Ninachokiona mimi ni muda mwafaka kuwa na mazungumzo na wadau wote wa demokrasia, haki za binadamu na utawala bora ili kwa pamoja tushinikize watawala (serikali) tushirikiane kuandika Katiba mpya ama kufanya marekebisho madogo," alishauri.
Alisema uchaguzi huo uliambatana na matukio mengi ambayo yaliashiria kukiukwa sheria za uchaguzi, ikiwamo kuandikisha watoto na marehemu kwenye daftari la wakazi, vyombo vya ulinzi na usalama kuhujumu uchaguzi kwa kuweka kura katika maboksi ya kura na hata kufanya mauaji.
Pambalu alisema matukio hayo yanapaswa kutumika kama funzo la kuona haja ya kufanya maboresho katika mifumo ya uchaguzi.
"Kwa hiyo, sisi kama chama (CHADEMA) tunatoa wito sasa, ni wakati sahihi kwetu wadau kuunganisha nguvu za pamoja kupigania Katiba itakayoleta haki na usawa katika masuala ya uchaguzi," alisema.
Pambalu alisema mabadiliko yoyote duniani hayakutokea kwa njia rahisi, bali kuna makundi ya watu yaliyojitoa mhanga ili kuleta mabadiliko hayo.
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Vijana wa Chama cha Wananchi (CUF), Iddi Mkanza, alitoa wito kwa mashirika kimataifa ya kidemokrasia kuingilia kati na kuwaunga mkono katika kuboresha demokrasia nchini.
Mkanza alisema kuwa ikiwezekana washirika wa maendeleo wasitishe misaada wanayotoa kwa Tanzania, akidai kuwa hivi sasa inanufaisha chama kimoja.
Alisema kuwa licha ya matokeo ya uchaguzi huo kuonesha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda kwa asilimia 99, kuna vijiji vingi ambavyo wagombea kutoka vyama vya upinzani walienguliwa na maeneo mengine wapigakura waliingia na kukuta wagombea ni wa chama kimoja.
"Tunahubiri demokrasia wakati kuna vitu vingi ambavyo haviendani na uhalisia, sisi kama chama (CUF) tunatarajia kutoa tamko kuhusiana na kilichotekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024," alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT - Wazalendo, Ester Thomas, alidai wananchi wanapaswa kutambua kuwa waliohujumu matokeo ya uchaguzi huo ni watumishi wa umma, likiwamo Jeshi la Polisi, walimu na watendaji wa vijiji na TAMISEMI ambayo ndiye msimamizi mkuu.
Alisema vyama vya siasa vilikuwa tayari kufanya marekebisho ya mifumo ya uchaguzi na ndio maana walijiunga katika kikosi kazi cha utekelezaji wake, lakini anahofu kama mapendekezo waliyotoa yanafanyiwa kazi au la.
Katibu Mkuu wa Chama cha Sauti ya Umma (CHAUMA), Majalio Kyara, alipongeza Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa kushirikisha vyama vya upinzani tangu mwanzo wa uchaguzi ingawa utekelezaji wa waliyokubaliana una mambo ambayo yaliwabana wakati wa uchaguzi huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED