SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limesema takribani watu 900 wameuawa na wengine 2,900 kujeruhiwa kutokana na mapigano yaliyodumu kwa siku saba katika mji wa Goma kati ya waasi wa M23 na Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Shirika la Uratibu wa Misaada ya Kiutu la Umoja wa Mataifa (OCHA) linasema, idadi hiyo ya watu 900 iliyotolewa na WHO katika ripoti yake, haijumuishi miili ya watu waliouawa kutokana na vita hivyo, ambayo iko kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti.
Inaelezwa kuwa miili ya watu bado imetapakaa katika mitaa ya mji wa Goma. Huku waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda wakitangaza kusitisha mapigano hayo kuanzia jana ili kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia katika mji wa Goma ulioshuhudia machafuko makali.
Wakati hayo yakijiri Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Rais wa DRC, Félix Tshisekedi wanatarajiwa kushiriki katika mkutano wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) Februari 8, mwaka huu jijini Dar es Salaam, ili kujadili mzozo huo.
Inaelezwa kuwa hatua ya M23 kusitisha mapigano inafuatia miito ya jumuiya hizo ili kuruhusu misaada ya kibinadamu kutolewa kwa maelfu ya watu walioachwa bila makazi katika mji wa Goma wenye wakazi takribani milioni tatu, huku milioni moja wakiwa wamekimbia makazi yao.
Usitishaji huo mapigano unajiri pia kuelekea mkutano wa kilele wa pamoja wa EAC na SADC wiki hii ambako Rais wa Kenya William Ruto amethibitisha kwamba Rais Kagame na Tshisekedi watahudhuria.
Inaelezwa kuwa viongozi hao wote wawili wamekuwa wakikwepa kuhudhuria mikutano ya awali ya kutafuta amani katika mzozo unaoendelea nchini Kongo.
Mamlaka nchini Kongo zinasema ziko tayari kwa mazungumzo ya kuleta amani ila mazungumzo hayo ni sharti yafanyike kwa muktadha wa makubaliano yaliyopita.
Waasi hao wanadaiwa sasa kuelekea katika mji wa Bukavu ingawa Jumatatu walithibitisha kwamba hawana nia ya kuuteka mji huo, huku wakisema awali kwamba wanapania kwenda katika Mji Mkuu Kinshasa.
KUHUSU MKUTANO
Rais Ruto ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC anasema mkutano wa jumuiya hizo unaotarajiwa kufanyika wiki hii nchini, umekuja baada ya viongozi wa jumuiya kwa nyakati tofauti kukubaliana kuwa na mkutano wa pamoja.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa endapo Rais Kagame na Rais Tshisekedi watahudhuria mkutano huo kama inavyotarajiwa itakuwa ni mara ya kwanza kukutana ana kwa ana tangu kundi la M23 lichukue mji wa Goma.
Katika kikao cha wakuu wa nchi za Afrika Mashariki kilichofanyika juma moja lililopita kwa njia ya mtandao, Rais Tshisekedi hakuhudhuria uamuzi ulioibua maswali ikiwa yuko tayari kwa mazungumzo ya kusaka suluhu ya kudumu kati yake na Rwanda.
Wataalamu wanaeleza kuwa mkutano huo wa wiki hii utakuwa wa muhimu hasa ikizingatia yanayoendelea kutokea na ambayo yanatishia usalama wa kikanda na kwamba ni lazima wakuu hao wa nchi watoke na azimio litakalosaidia kupatikana kwa suluhu ya kudumu.
Mji wa Goma uko katikati ya eneo lenye utajiri wa madini ikiwemo shaba, cobalt, dhahabu na coltan yanayotumika kutengeneza simu za rununu na betri za magari ya umeme, unasalia kuwa chini ya udhibiti wa waasi wa M23 wanaoripotiwa kusonga mbele na kuchukua udhibiti wa maeneo mengine ya mashariki mwa DRC.
HALI ILIVYO
Inaelezwa kuwa kwa sasa, Goma ndio mji ambao M23 wanajivunia kuuteka. Huku hali ya eneo hilo ikionyesha taswira vile hali itakavyokuwa iwapo waasi hao wataendelea kuteka na kudhibiti miji mingine zaidi.
Kadhalika inaelezwa kuwa wengi wa wananchi wanasema wameanza kuzoea kutawaliwa na kundi la M23.
Vile vile, taarifa zinaeleza kuwa waasi hao walifanikiwa kudhibiti hadi ofisi ya Gavana wa kijeshi wa Kivu Kaskazini, ambaye walimuua walipokuwa wakiingia na kuvamia mji wa Goma.
Pia inabainishwa kuwa wapiganaji walikuwa wakishika doria katika maeneo mbalimbali katika eneo hilo, huku wengine wakizunguka mjini wakiwa wamebeba silaha.
Kutokana na hali hiyo inaelezwa kuwa watu wengi bado wana wasiwasi wakihofia uwezekano wa kurejea kwa mapigano katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
Mmoja wa wakazi muuza duka katika mji wa Goma Sammy Matabishi anasema “Watu wanauoga...bado nina hofu kwasababu wale walioleta vurugu bado wako miongoni mwetu na hatujui kinachoendelea kwa sasa.”
“Lakini cha kushangaza zaidi ni kuwa hakuna anayekuja kununua bidhaa madukani mwetu, wengi wamehamia Rwanda, mji ulioko mpakani na Kongo Bukavu, Kenya na Uganda,” anasema.
Wakati huo, M23 wakisherehekea ushindi mkubwa licha ya kutangaza kusitisha mapigano, serikali ya Kongo inaendelea kukataa madai kwamba waasi hao wameuteka kikamilifu mji wa Goma.
Mamlaka ya DRC imekuwa ikiwashutumu M23 kwa kuchukua ardhi yao kinyume cha sheria kwa madai ya kupatiwa msaada na Rwanda, huku ikiahidi kurejesha maeneo yaliyopotea.
Ingawa Rwanda imekuwa ikikanusha mara kwa mara kuhusika na kuunga mkono waasi wa M23, majibu yake yameanza kugeuka na kuwa ya kujitetea, huku msemaji wa serikali hiyo akieleza kuwa vita vinavyoshuhudiwa karibu na mpaka wao ni tishio kwa usalama wao.
Waasi sasa wanadaiwa kusogea kusini kuelekea Bukavu, mji mkuu wa Kivu Kaskazini, na wameapa kufika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kinshasa.
UNYANYASAJI
Wakati mashariki mwa Kongo inakumbwa na misukosuko ya kisiasa, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa inatahadharisha kuwa unyanyasaji wa kijinsia unatumika kama silaha ya vita na pande pinzani.
Daktari katika moja ya hospitali binafsi katika eneo hilo alithibitisha kauli ya Umoja wa Mataifa, akisema taasisi yake imepokea hadi sasa waathiriwa 10 wa ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia.
Inaelezwa kuwa ingawa milio ya risasi na milipuko mjini Goma imepungua, sio maeneo yote ambayo shughuli za kila siku zimerejea kama kawaida.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED