Yaliyombeba Samia sekta ya afya hadi kutunukiwa tuzo

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 10:02 AM Feb 05 2025
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan amepokea tuzo ya heshima ya ‘The Gates Goalkeepers Award’ kutambua juhudi zake za kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa asilimia 80, kuboresha upatikanaji huduma za afya na kukuza usawa wa kijinsia katika sekta hiyo.

Kiongozi huyo anakuwa wa saba duniani na wa kwanza Afrika kutunukiwa tuzo hiyo ambayo hutolewa kwa viongozi waliowezesha nchi zao kuharakisha maendeleo kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG).

Kutokana na tuzo hiyo iliyotolewa na Taasisi ya The Gates Foundation, Rais Samia katika hotuba yake jana Ikulu, jijini Dar es Salaam, aliainisha maendeleo ya nchi katika kuboresha huduma za afya na lishe na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika mifumo inayozingatia utu wa kila mtu.

Rais Samia alitoa tuzo hiyo kwa wafanyakazi wa sekta ya afya kama njia ya kukubali kujitolea kwao bila kuchoka na kuainisha maeneo kadhaa yaliyochangia nchi kuipata na kazi inazoendelea kufanya.

"Tuzo hii ni ya kutia moyo kwa sababu nyingi, hasa Gates Foundation, pamoja na kuwa mdau muhimu katika ajenda ya kimataifa ya afya, imeendelea kuwa mshirika muhimu wa Tanzania," alisema.

Rais Samia alisema tuzo hiyo ni utambuzi wa uongozi wa pamoja na dhamira ya watanzania wanaofanya kazi bila kuchoka kuboresha maisha ya wanawake, watoto na familia na kusisitiza uboreshaji lishe umekuwa msingi wa ajenda ya nchi kwa maendeleo ya taifa.

Rais Samia alieleza namna nchi ilivyowekeza katika afya ya uzazi, uwekezaji kwenye vituo vya afya na watumishi na kutoa kipaumbele kwa afya ya mama na mtoto.

"Tangu mwaka 2021 (alipoingia madarakani), tumechukua hatua mbalimbali za kuboresha afya ya uzazi, mtoto mchanga na vijana wanaobalehe pamoja na lishe.

"Inatia moyo kuona kwamba kutokana na afua mbalimbali za kimkakati, uwiano wa vifo vya uzazi umepungua kama inavyosemwa hapa. Lakini pia, vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano vimepungua kutoka asilimia 67 hadi asilimia 43 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa, ni matokeo ya juhudi za pamoja," alisema.

Rais Samia alisema wameongeza idadi ya madaktari bingwa waliosajiliwa kutoka 69 mwaka 2020 hadi 338 mwaka 2024.

"Tumekuwa tukitoa huduma za afya za uzazi bila malipo na kwa watoto chini ya miaka mitano. Pia tumeimarisha mifumo ya rufani kwa kuongeza magari 727 ya wagonjwa katika kipindi cha miaka tisa kuanzia 2015 hadi 2024 na hivyo kuimarisha upatikanaji huduma za dharura za uzazi kwa kuziba pengo kati ya jamii za vijijini na vituo vya afya," alisema.

Rais Samia alisema wameanzisha pia huduma za rufani za dharura za mama na mtoto aliyezaliwa na kuongeza idadi ya mashine za ultrasound kutoka 345 mwaka 2020 hadi 970 mwaka 2024.

Pia alizungumzia ujenzi mkubwa wa barabara za vijijini ili kurahisisha safari za kwenda na kurudi kwenye vituo vya afya.

"Nne, tumesaidia katika kuendeleza TEHAMA ili kufanya tathmini ya vifo vya kinamama wajawazito na matokeo yake ni kutambua uwezo wa kudhibiti baadhi ya matatizo ya uzazi na imeongeza juhudi za kuimarisha kujenga uwezo kupitia ushauri kwa watoa huduma za afya.

"Tano, serikali ilianzisha mikakati ya kisekta, ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia, tathmini ya lishe kwa kununua mashine ambazo zimeimarisha uwezo wa taifa kufanya uchambuzi unaohusiana na lishe, kama vile matumizi ya sampuli za kibaolojia ili kupata hali ya lishe kwa kutumia utaalamu wa ndani.

"Udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano umepungua kutoka asilimia 42 mwaka 2015 hadi asilimia 30 na uzito mdogo umepungua kutoka asilimia 16 hadi asilimia 12 katika kipindi hichohicho," alisema.

Rais Samia alisema bado wanaendelea kuchukua hatua zinazohitajika ili kupunguza uzito mdogo, udumavu na utapiamlo.

Mkuu wa Nchi pia aliangazia juhudi zinazoendelea za kushughulikia afya ya vijana, hasa kwa kuzingatia kuzuia mimba za utotoni kunakolenga kukabiliana na vikwazo vya kitamaduni na kimila, ili kuhakikisha maisha ya baadaye ya afya kwa vijana wa taifa hilo.

Alisema matokeo ya juhudi hizo, mimba za utotoni zimepungua kutoka asilimia 27 hadi asilimia 22.

"Sita, kupelekwa kwa wafanyakazi wa afya ya jamii ambao wamekuwa muhimu wanaohakikisha kunakuwa na upatikanaji huduma muhimu za afya katika ngazi ya chini na kuwa kiungo muhimu kati ya vituo vya afya na jamii kutoa elimu muhimu ya afya na kukuza chanjo na lishe programu," alisema.

Alisema wamechangia katika ongezeko la ufahamu na kushughulikia vikwazo kama vile mila na desturi za kitamaduni.

"Bado tuna kazi ya kufanya ili kuboresha zaidi huduma za afya, zaidi ya hayo, changamoto zingine kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, milipuko ya kikanda na ukosefu wa usawa wa kiuchumi zinatukumbusha kwamba kazi yetu lazima iendelee kwa nguvu mpya," alisema.

Rais wa Usawa wa Kijinsia kutoka Taasisi ya Gates Foundation, Anita Zaidi alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika afya ya mama na mtoto katika miaka kadhaa iliyopita.

"Kupitia mifumo iliyoimarishwa ya huduma za afya, kuboreshwa kwa upatikanaji huduma za uzazi na kuzingatia matunzo bora, kinamama wengi zaidi wananusurika wakati wa kujifungua na watoto wengi zaidi kuwa na fursa ya kustawi," alisema.

Anita alibainisha kuwa dhamira ya Tanzania katika SDG, ambayo ilitia saini mwaka 2015, imeiweka kuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengine.

"Kuanzishwa kwa mipango kama vile programu ya M-MAMA, ambayo inahakikisha wajawazito wanapata usafiri wa dharura hadi kwenye vituo vya afya, ni mfano mmoja wa mbinu za maendeleo ya nchi," alisema.

Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, alisema tuzo hiyo ni uthibitisho wa uongozi wa kipekee wa Rais Samia na dhamira isiyoyumba katika kuboresha huduma za afya.

APOKEWA DODOMA

Muda mfupi baada ya kupokea tuzo hiyo, Rais Samia alikwenda Makao Makuu ya Nchi jijini Dodoma, alikopokewa na viongozi wa serikali na chama na kuwaeleza kuwa dunia imetambua jitihada za serikali katika huduma za afya hasa kwa kinamama.

Alikumbushia kuwa miaka minne iliyopita vifo vilivyotokea wakati wa kujifungua vilikuwa 556 kati ya wajawazito 100,000 waliofika hospitalini kupata huduma ya uzazi.

"Lakini kwa sababu tumefanya uwekezaji mkubwa kwenye afya, kwa kujenga majengo mengi, upatikanaji vifaa tiba na kusomesha wafanyakazi, tumepunguza vifo kutoka 556 mpaka 104 kati ya wajawazito na malengo ya dunia ifikapo mwaka 2030 tuwe na vifo 70 tu na tunaamini tutafika huko na tutavuka lengo.

"Lakini kwa watoto chini ya miaka mitano tumepunguza vifo japo tuna kazi kubwa ya kufanya kwa wanaozaliwa, tulikuwa tunawapoteza kwa mambo kadhaa ikiwamo matumizi ya dawa za kienyeji, kuchelewa kufika hospitalini pamoja na kukosa vifaa vya kuokoa maisha yao," alisema Rais Samia.