WATU wanne wamehukumiwa kifungo cha maka 42 gerezani baada ya kupatikana na hatia katika kesi namba 5,537 ya mwaka 2024 ya kuvunja duka na wizi wa sigara, vocha na simu.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Tunduru, Shughuli Mwampashe baada ya kujiridhisha bila shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri katika shauri hilo.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mwampashe alisema mshtakiwa namba tatu na namba nne wanahukumiwa kifungo cha miaka 24 gerezani na mshtakiwa na namba mbili anahukumiwa kifungo cha miaka 18 gerezani baada ya kusikiliza ombi lao.
Waliohukumiwa kutumikia adhabu hiyo ni Sophia Mtewa aliyekutwa na hatia ya kuwapokea washtakiwa na kuwaficha nyumbani kwake wakati wakitekeleza uhalifu huo.
Wengine ni Hamis Mchivali, Mfaume Namangwalu na Salum Hassan aliyewahifadhi nyumbani kwake ili wasikutane na mkono wa sheria licha ya kufahamu kuwa ni wahalifu.
Washtakiwa watatu walikuwa wanakabiliwa na mashtaka manane, mmoja akikabiliwa na shtaka moja. Shtaka la kwanza na la tatu ni kwa mshitakiwa namba mbili na tatu kwa kosa la kuvunja jengo na wizi kinyume cha kifungu cha 299(a) na (b) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura 16.
Ilidaiwa mahakamani huko na Mwendesha Mashtaka, Inspekta Ernest Machiya kwamba Agosti 6, 2024, katika kijiji cha Cheleweni, wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma, washtakiwa walivunja na kuingia katika duka la Mussa Mpanjikwa kwa nia ya kutenda kosa la wizi.
Alidai kuwa mara baada ya kuvunja na kuingia katika duka hilo, washtakiwa hao waliiba simu janja moja aina ya Sumsang Galaxy A3 yenye thamani ya Sh. 534,000, mali ya Mussa Mpanji
Katika shtaka la tatu, washtakiwa walidaiwa kuvunja na kuingia katika duka la Yona Mligo kwa nia ya kutenda kosa la wizi, huku katika shtaka la nne, kwa pamoja walidaiwa kuvunja, kuingia na kuiba simu mbili, moja aina ya TECNO T 301 yenye thamani ya Sh. 30,000 na nyingine aina ya Oking yenye thamani ya Sh. 30,000, mali ya Yona Mligo.
Kwa mujibu wa Inspekta Machiya, katika shtaka la tano, mara baada ya kuvunja na kuingia ndani ya duka, washtakiwa waliiba simu aina ya Tecno T 528, mali ya Seleman Hassan yenye thamani ya Sh. 50,000 katika duka la Yona Mligo.
Katika shtaka la sita, walidaiwa kuvunja na kuingia ndani ya duka na kuiba simu moja aina ya Tecno Pop 5 yenye thamani ya Sh. 180,000, mali ya Hamis Tawakali.
Mwendesha mashtaka alidai kuwa katika kosa la saba na la nane, mshtakiwa namba nne alipatikana na mali isiyo halali kinyume cha kifungu cha 312(1)(b) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura 16 Agosti 7, 2024 katika kitongoji cha Kigamboni, wilayani Tunduru.
Ilidaiwa mahakamani huko kuwa washtakiwa hao walipatikana na pakti 13 za sigara aina ya Winston zenye thamani ya Sh. 39,000, pia pakti saba zingine za Winston za rangi nyekundu zenye thamani ya Sh. 21,000, pakti moja ya sigara aina ya Sports yenye thamani ya Sh. 5,000, pakti 10 za sigara aina ya Master Menthol za Sh. 30,000, pakti 19 za sigara aina ya Master Filter zenye thamani ya Sh. 57,000.
Washtakiwa hao pia walidaiwa kukutwa na pakti sita za sigara aina ya Clessent na Star, zote zina thamani ya 170,000.
Katika shtaka la nane, washtakiwa walidaiwa kukutwa na mali isiyo halali; vocha za mitandao ya simu tofauti, vocha 35 za Vodacom za Sh. 500, vocha 60 za TTCL za Sh. 500, vocha 66 za Halotel za Sh. 500 na vocha 53 za Airtel za 500, zote zikiwa na thamani Sh. 107,000.
Mshtakiwa namba moja alidaiwa kushirikiana na wahalifu kwa kuwahifadhi kinyume cha sheria, akikiuka kifungu cha 388 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura 16.
"Mnamo Agosti 6, 2024, mshtakiwa namba moja kwa jina Sophia Rajabu Mtewa, aliwapokea washtakiwa Hamis Mchivali, maarufu Chake, Mfaume Mussa Namangwalu na Salum Said Hassan, maarufu kama Kanda, akiwa na ufahamu kwamba ni wahalifu na kuwahifadhi ili wasikutane na mkono wa sheria," alidai.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED