STENDI YA MAGUFULI- Ulivyo mtihani wa usafi vyooni kuanzia abiria hadi walio kazini

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 12:26 PM Feb 05 2025
Mwonekano wa nje wa vyoo vya wanawake katika stendi hiyo.
Picha: Christina Mwakangale
Mwonekano wa nje wa vyoo vya wanawake katika stendi hiyo.

LICHA ya kulipia huduma, maelfu ya abiria wanaotumia Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, mkoani Dar es Salaam, wako hatarini kupata magonjwa, yakiwamo maambukizi katika mfumo wa mkojo (UTI), kutokana na vyoo vya stendi hiyo kuwa kwenye mazingira machafu.

Stendi ya Magufuli ni moja ya vituo bora vya mabasi nchini na Afrika Mashariki. Ujenzi wake uligharimu Sh. bilioni 50, ina matundu 140 ya vyoo. Kati yake, 56 ni kwa ajili ya wanaume.

Hata hivyo, ni jambo la kawaida kukuta maji yametuama kwenye sakafu za vyoo vya stendi hiyo. Hali ni mbaya zaidi upande wa vyoo vya wanawake, ambavyo havina vyombo maalum vya kutupa taka ngumu, zikiwamo taulo za kike, ndoo za kuhifadhia maji zimechakaa na makopo yanayotumika ni dumu la lita tano, ambalo limekatwa.

Kituo hicho, kama ilivyotolewa ufafanuzi na uongozi wake, kinahudumia wastani wa abiria 16,000 hadi 20,000 kwa siku. Hao ni mbali na wanaokwenda kusindikiza au kuwapokea ndugu zao, wafanyakazi wa mabasi na wafanyabiashara ndogo.

Watumiaji hao wa kituo hicho wanatakiwa kulipa ushuru wa aina mbili; kwanza Sh. 300 ya kiingilio cha getini kwa wale ambao hawana tiketi za mabasi na Sh. 200 kwa kila anayehitaji kwenda msalani kujisaidia.

Mbali na abiria na wasindikizaji wao, pia kuna makundi mengine ya watumiaji huduma za msalani kituoni huko ni vibarua wasukuma matoroli ya kubeba mizigo, wajasiriamali wadogo ambao kwa pamoja wanafikia 360.

Doreen Mwakabuta, ambaye anajitambulisha ni msafiri wa mara kwa mara anayetumia kituo hicho kwenda mikoa tofauti nchini, anasema kila anapofika kituoni huko, hulazimika kuwa na tafakuri ya muda kuingia msalani, akihofia kupata magonjwa kama vile UTI.

"Unajua kwa wanawake, magonjwa ya mfumo wa mkojo ni rahisi kuambukizwa iwapo choo si safi. Binafsi nikiingia katika choo chenye majimaji yaliyosambaa sakafuni, kinatoa harufu, huwa ninakosa raha, nitajisaidia kwa shida," anasema.

Doreen ana lingine la ziada -- vyoo hivyo si rafiki kwa matumizi ya watu wenye ulemavu. Ujenzi wake haukuzingatia mahitaji ya kundi hilo.

Dereva wa basi linalofanya safari kati ya Dar es Salaam na Songea, Ayubu Mambosasa, anasema kampuni anayofanyia kazi, ina ofisi nje ya kituo hicho cha mabasi, hivyo ni mara chache huingia kutumia vyoo vya stendi hiyo.

"Ninaingia chooni mara chache, labda nibanwe sana kwa sababu ninajua kitu chenye matumizi mengi, lazima kina changamoto. Usafi ni mdogo, ila nikibanwa ninaingia, sina namna," anasema dereva huyo.

Geofrey Godson ni msukuma toroli anayesaidia abiria kubeba mizigo yao katika stendi hiyo. Anasema amefanya kazi hiyo kwa miaka miwili, kazi anayoitaja inamwezesha kuendesha maisha yake.

"Huduma ya choo ni Sh. 200 kila unapohitaji huduma. Na kwetu sisi ambao tuko chini ya kampuni tunavaa sare, lakini tunalipia isipokuwa getini tu ndiko hatulipii kwa sababu tuna hizi sare. Kuna wakati huwa ninajibana nisinywe maji mengi, ili nisiende msalani mara nyingi.

"Lakini kwa kuwa sisi ni wanaume, unaweza kwenda sehemu ukajibanza kujisaidia haja ndogo hata katika chupa ya maji, unaiacha hapo hapo. Fedha ninayopata kwa siku haizidi Sh. 20,000, hapo kuna Sh. 11,000 ya bosi, ninywe chai, chakula mchana na usiku," Godson anasimulia. 

Amina Shaban, mchuuzi katika kituo hicho kwa miaka mitatu sasa, akiuza bidhaa ndogo kama karanga, pipi, biskuti, maji na juisi, anasema kuwa kila siku anapoingia getini alfajiri hulipia Sh. 300 na anapoingia msalani hulipia Sh. 200.

"Hiyo Sh. 200 unalipa kila unapoingia msalani. Pale tumbo linapovurugika ndipo gharama inakuwa kubwa zaidi na biashara ni ya kawaida si nzuri, faida ni ndogo bado, sijala, sijanywa maji. Inabidi kuwa makini na unywaji wako wa maji.

"Hata ukibanwa inabidi ujibane kidogo. Kwa ujumla kama unashinda humu, suala la maji ya kunywa hatulipi kipaumbele. Kwa sababu chai asubuhi si chini ya Sh. 1,000, chakula cha mchana labda Sh. 1,500, bado usiku urudi nyumbani ukapike, biashara yenyewe iko wapi?" Amina anahoji.

Wakati baadhi ya wachuuzi katika Stendi ya Magufuli wakijizuia kunywa maji kwa hofu ya gharama za ushuru wa huduma ya choo, Bingwa wa Magonjwa ya Figo na Mfumo wa Mkojo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Jonathan Mngumi, anaonya kuwa mtu yeyote anayefanya kazi nzito juani au inayomfanya atokwe jasho jingi, ana kiwango maalum cha unywaji maji.

"Kwa wastani mtu mzima anayefanya kazi nzito juani au kazi ya kutoka jasho jingi, anashauriwa kunywa maji kati ya lita tatu hadi tano kwa siku kulingana na kiwango cha jasho na unyevunyevu wa mazingira.

"Kujinyima kunywa maji na uko kwenye mazingira hayo si sahihi. Kila baada ya saa moja ya kufanya kazi nzito, kunywa takriban mililita 500 mpaka lita moja ya maji. 

"Ikiwa mtu anajisikia kiu sana au mkojo wake ni wa rangi ya njano iliyokolea, ni dalili ya upungufu wa maji mwilini na anapaswa kuongeza unywaji maji.  Athari za unywaji maji usio sahihi ni pamoja na kuathiri viungo kadhaa muhimu; figo kushindwa kufanya kazi ipasavyo na hata kukumbwa na UTI, ngozi kuwa kavu na kuzeeka haraka. 

"Vilevile, moyo huongeza mzigo kwa sababu ya kupungua kwa ujazo wa damu, ubongo unaweza kusababisha maumivu ya kichwa, kutoelewa vizuri na uchovu.

Vifaa vinavyotumika msalani katika Stendi ya Mabasi ya Magufuli. PICHA: CHRISTINA MWAKANGALE
"Unywaji duni wa maji pia husababisha mmeng'enyo wa chakula kuwa duni, husababisha kufunga haja kubwa na kuongeza asidi tumboni, jambo linaloweza kusababisha vidonda vya tumbo," bingwa huyo anatoa tahadhari. 

Dk. Mngumi ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Figo na Bingwa wa Magonjwa ya Figo MNH, anasema kwa wastani mtu hujisaidia haja ndogo mara nne hadi saba ndani ya saa 12 hadi 24, sawa na wastani wa kupata haja hiyo kila baada ya saa tatu hadi nne.

"Unywaji duni wa maji huathiri mfumo wa mkojo kuanzia kwenye figo hadi kibofu, huongeza uwezekano wa maambukizi ya UTI, hasa kwa wanawake. Hupunguza uwezo wa kibofu kufanya kazi ipasavyo, jambo linalosababisha hisia ya haja ndogo," bingwa huyo anaonya.

Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (TAKUHA), Solomoni Nkigi, anasema abiria wa makundi yote wana haki ya kupata huduma bora mahali popote, ikiwamo vituo vya abiria.

"Nipashe mmefanya uchunguzi wenu, na sisi tunakwenda kufanya uchunguzi kuhusu vyoo, maana kituo kimejengwa na huduma kama hizo tunaona kama zinakidhi," anasema.

Richard Shumbusho, Mwanasheria kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), anatoa fasili ya huduma ya choo kisheria.

Anasema huduma ya choo ni muhimu kwa sababu inazuia magonjwa, inaboresha usalama na inasaidia maendeleo ya kiuchumi. Hivyo ni jukumu la serikali kulinda haki hiyo, ili kuhakikisha kila mtu anapata huduma bora, safi na salama kwenye maeneo ya mkusanyiko kama stendi hiyo ya mabasi.

"Ni muhimu kuhakikisha kwamba ada hizi (zinazotozwa) hazizuii watu kupata huduma muhimu na kwamba zinatumika kwa ajili ya kuboresha huduma hizo. Serikali inapaswa kuhakikisha kunakuwa na huduma ya choo bora kwa wote bila kujali uwezo wa kifedha wa wahitaji," anasema.

Mwanasheria huyo anasema Ibara ya 138(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inaelekeza ada na ushuru wowote lazima uanzishwe kwa mujibu wa sheria.

"Malipo yanayotozwa kwa huduma za choo, yanapaswa kuwa na msingi wa kisheria, ili kuhakikisha haki za wananchi zinaheshimiwa. Kwa hiyo ada hizi ni muhimu katika kuhakikisha huduma za choo zinapatikana zikiwa salama na zenye ubora kwa watumiaji wote," anasema.

Meneja wa Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Isaac Kasebo, anasema huduma zinazotolewa kituoni huko kama vile choo zinalipiwa ili kuwa endelevu na bora.

"Changamoto iliyopo kwenye huduma za vyoo ni baadhi ya watumiaji kuharibu miundombinu ya vyoo, jambo linalosababisha upotevu wa maji na matengenezo ya mara kwa mara.

"Jumla ya matundu ya vyoo ni 140 (84 ya wanawake 84) na hufanyiwa usafi muda wote. Maji yanapatikana, tunahifadhi akiba kwenye matangi ya lita 500,000 pia tumejenga kisima kinachotumika pindi maji ya DAWASA (Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam) yanapokatika," meneja huyo anasema.

Kasebo anaeleza kuwa msimu wa mwisho wa mwaka na sikukuu, abiria huongezeka na kufanya kiwango cha mapato pia kuwa juu kutoka wastani wa Sh. milioni nane hadi Sh. milioni 10 kwa siku.

"Vyanzo vya mapato haya ni kutokana na ushuru tofauti, kama vile vyoo, getini, mabasi na pango. Mabasi yanayotoa huduma kwa siku ni kati ya 170 na 200. Wasafiri kwa siku hutegemeana na misimu. Kwa mfano kipindi cha abiria wachache, wanakuwa wa wastani wa abiria 16,831, msimu wa abiria wengi, tunakuwa na wastani wa abiria 20,874," anasema.

*ITAENDELEA KESHO