BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Ushetu, mkoani Shinyanga, limepitisha makadirio ya bajeti ya Shilingi bilioni 41.2 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, huku likiwahimiza wakulima wa mazao ya biashara kutojihusisha na utoroshaji wa mazao ili kufanikisha lengo la makusanyo hayo.
Aidha, baraza hilo limependekeza kuajiri watumishi wapya 436, kupandisha vyeo au madaraja watumishi 697, na kubadilishiwa madaraja watumishi 19.
Bajeti hiyo iliidhinishwa Februari 4, 2025, katika kikao cha Baraza la Madiwani la Ushetu, ambapo madiwani waliipongeza serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo, hasa ile iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi katika sekta za afya na elimu.
Akiwasilisha makadirio hayo, Ofisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Shigela Ganja, alisema bajeti hiyo imeongezeka ikilinganishwa na ile ya mwaka 2024/25, ambayo ilikuwa Shilingi bilioni 35.5, ikijumuisha mapato lindwa na yasiyolindwa.
Alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026, halmashauri inatarajia kukusanya Shilingi bilioni 41.2, ambapo mapato ya ndani yasiyolindwa ni Shilingi bilioni 3.85, miradi ya maendeleo Shilingi bilioni 1.5, matumizi mengineyo Shilingi bilioni 2.3, ruzuku ya mishahara Shilingi bilioni 25.6, ruzuku ya miradi Shilingi bilioni 9.36, ruzuku ya serikali Shilingi bilioni 4.6, na michango ya wananchi Shilingi bilioni 4.6.
Diwani wa Viti Maalumu wa Kata ya Bulungwa, Ester Matone, alihimiza halmashauri kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuboresha vilivyopo, kwani asilimia kubwa ya mapato yanategemea zao la tumbaku ikilinganishwa na mazao mengine ya biashara.
Naye Diwani wa Nyamilangano, Robert Mihayo, alisisitiza umuhimu wa kudhibiti utoroshaji wa mazao ili kufanikisha malengo ya makusanyo. Alisema kila diwani anapaswa kuhakikisha suala hilo linasimamiwa ipasavyo ili kufanikisha makusanyo kwa zaidi ya asilimia 100, kama ilivyofanikishwa mwaka wa fedha 2023/2024.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED