BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza application 69 ambazo haziruhusiwi kutoa huduma za mikopo mtandaoni kwa kuwa hazina kibali na haziruhusiwi kuendesha shughuli hizo, huku ikiitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzifungia.
Hatua hii inakuja mwezi mmoja tangu Nipashe iibue kero iliyopo kwenye mikopo mtandaoni, huku kasi ya udhalilishaji na utoaji riba kubwa ambao hauna utaratibu wa kisheria hadi BoT ilivyotoa mwongozo kwa watoa huduma hao na kuwataka wajisajili.
Licha ya kupewa siku 14, walijitokeza waombaji 16 na kati yake 14 pekee walikidhi vigezo, huku BoT ikichukua hatua kali kwa Microfinance ambazo zilianzisha Apps na kutoa mikopo mtandaoni.
Taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba: “Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuufahamisha umma kuwa imebaini kuwepo kwa Majukwaa na Programu Tumizi ‘Applications” zinazojihusisha na utoaji wa mikopo kidijitali bila ya kuwa na leseni na idhini kutoka Benki Kuu ya Tanzania.”
Kupitia taarifa hii, Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuuarifu Umma kwamba Majukwaa na Programu Tumizi “Applications” zifuatazo hazina kibali na haziruhusiwi kuendelea na shughuli za utoaji mikopo kidijitali.
Application hizo ni BoBa Cash; Hewa Mkopo; Money Tap; Soko loan; Bolla Kash Financial Credit; Hi Cash; Mpaso chap loan-Mkopo kisasa; Sunloan; BongoPesa-Personal Online Loan; HiPesa; Mun loan; Sunny Loan na Cash Mkopo.
Wengine ni Jokate Foundation Imarisha Maisha; My credit; Swift Fund; Cash pesa; KOPAHAPA; Nikopeshe App; TALA; Cash poa; Kwanza loan; Nufaika Loans; TikCash; CashMama; L-Pesa Microfinance; Okoa Maisha – Mkopofast na Twiga Loan.
Wengine ni CashX; Land cash; Pesa M; TZcash; Credit Land; Loanplus; Pesa Rahisi; Umoja; Eaglecash TZ; M-Safi; PesaPlus 64. Usalama Na Uwakika Mkopo Dk15; Fast Mkopo 29.
Wengine Mkopo Express; PesaX ; Ustawi loan; Flower loan; Mkopo Extra; Pocket loan; Viva Mikopo Limited; FUN LOAN; Mkopo haraka; Pop Pesa; VunaPesa; Fundflex; MkopoFasta; Premier loan; Yes Pesa; Get cash.
Wengine ni MkopoHaraka; Safe pesa; ZimaCash; Getloan; Mkopohuru; SasaMkopo; Getpesa Tanzania; Mkoponafuu; Silk loan; Hakika loan; Mkopowako; na Silkda Credit.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa Nipashe kwa miezi minne, ulibaini utoaji mikopo mtandaoni kiholela.
Ni mikopo yenye riba kubwa inayofika hadi asilimia 80, masharti ya mikopo yanafichwa, udhalilishaji wakopaji kwa kuundiwa makundi katika mitandao ya kijamii kisha picha zao kusambazwa, matumizi ya namba za simu zenye utambulisho (code) usiotambulika.
Mwandishi pia amebaini vijana wenye umri mdogo wamekuwa wanatumika kutukana na kudhalilisha wakopaji kwa njia ya simu, kutuma na kusambaza picha chafu zilizotengenezwa kwa lengo la kushinikiza mkopaji kulipa kiasi kisichostahili, wakopaji kupewa mkopo pungufu kinyume cha makubaliano ya awali na kuwapo raia wa China wanaotumia teknolojia kutoa mikopo.
Katika uchunguzi wake, mwandishi pia amebaini wakopeshaji wana watumishi wanaodai kulipwa ujira kwa kadri wanavyokusanya, ofisi feki za wanaotoa mikopo na matangazo yenye udhamini katika mitandao ya kijamii.
Vilevile, mwandishi amebaini kuwa mara baada ya mkopaji kutoa rukhsa ya taarifa zake binafsi kujulikana, wakopeshaji wanakuwa na uwezo wa kuingia katika akaunti yake ya Google na kuona mawasiliano yote kisha hutuma ujumbe ndani ya dakika moja, kwa watu wote walio katika orodha ya simu ya mkopaji kuwaarifa kuwa “huyu anadaiwa”.
Uchunguzi pia umebaini wakopeshaji wanaingilia na kuendesha mawasiliano ya mtu, jambo ambalo limekuwa chanzo cha utapeli ukiwamo wa “zile fedha tuma katika namba hii”.
Wakopeshaji hao wanakwenda mbali zaidi, kuna wakati wanavunja ndoa na baadhi ya watu kuripotiwa kujiua kutokana na madeni yasiyolipika; yanakuwa na riba inayoongezeka bila ufafanuzi rasmi.
Mwandishi alibaini hakuna mwongozo wala sheria ya kuwadhibiti hadi BoT ilivyotangaza mwongozo huo Septemba, mwaka huu. Ni hatua iliyopunguza kasi ya matangazo ya wakopeshaji hao katika mitandao ya kijamii, lakini baada ya wiki moja, matangazo hayo yalirejea kwa kasi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED