MAMLAKA ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji na Mauzo nje ya Nchi (EPZA), imewataka wawekezaji wa ndani na nje kuchangamkia fursa kubwa katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zitokanazo na korosho kwa ajili ya kuuza nje ya nchi na kuchangia pato la taifa na uchumi wa nchi.
Tanzania inasifika kwa kuwa na korosho nzuri duniani ambazo zinawahakikishia wawekezaji kupata soko la uhakika kimataifa hasa zinapoongezwa thamani.
Tanzania imeweka mkakati wa kuongeza uzalishaji wa korosho hadi kufika tani milioni moja ifikapo mwaka 2030, mpango ambao utaongeza uchangiaji wa sekta ya kilimo katika uchumi wa nchi.
Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji wa EPZA, James Maziku, alisema hayo wakati walipotembelea kiwanda cha kuchakata korosho cha Tan Ko Mirae Green Company kutoka Korea kilichopo wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani kuwa kuna fursa kubwa katika uchakataji wa korosho ambao unamhakikishia mwekezaji kupata faida kubwa.
“Nawahimiza wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika uchakataji wa korosho hasa kupitia Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo Nje (EPZ) na Maeneo Maalum ya Kiuchumi ya (SEZ) kwani yanawapa uhakika wa kupata faida kubwa,” alisema.
Alisema katika ziara hiyo walitembelea viwanda sita katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani hasa Wilaya ya Mkuranga ikiwa ni mwendelezo wa kukagua na kufanya tathmini ya viwanda ambavyo vimepewa leseni na EPZA zaidi ya 200 nchini.
Maziku alisema mamlaka ya EPZA huvutia na kusajili viwanda kwa ajili ya kuzalisha bidhaa kwa mauzo nje ya nchi ili kuongeza fedha za kigeni katika nchi huku ikichangia kuongeza ajira, teknolojia mpya na kuhakikisha kuwa bidhaa za mazao haziuzwi nje zikiwa ghafi.
Meneja wa Uendeshaji wa Kiwanda cha Tan-Ko Mirae Green, Eric Nkanda, alisema kuwa kiwanda hicho hadi sasa kimeajiri wafanyakazi 45 na pia kinachangia kipato kwa kiasi kikubwa kwa wakulima wa korosho katika mikoa ya Lindi, Mtwara na wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani.
Hata hivyo, Nkanda alisema mgawo wa umeme ni tatizo kubwa na kuongeza gharama za uzalishaji kutokana na matumizi ya mafuta kwenye majenereta.
Kiwanda cha kuchakata korosho cha Tan Ko Mirae Green Company ambacho uwekezaji wake ni zaidi ya Dola za Kimarekani milioni tano, kilizinduliwa mwezi Desemba, mwaka jana kikiwa na uwezo wa kuchakata kati ya tani 3,000 na 4,000 za korosho kwa mwaka.
Pia, kiwanda huzalisha mafuta maalum mazito ambayo ni rafiki kwa mazingira kwa ajili ya matumizi kwenye mitambo ambayo yote soko lake lipo nchini Korea.
Kiwanda pia huzalisha kati ya tani 2,500 hadi 3,000 za mkaa kwa mwaka pamoja na bidhaa za mbolea.
Katika ziara hiyo, Mamlaka ya EPZA ilitembelea kiwanda cha kuchakata chupa tupu cha plastiki, LVDI International Enterprise Limited kilichopo Temeke, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Wang Lingang, alisema hadi sasa kimeajiri watu 85 kwa mikataba na vibarua 54.
Alisema soko lao kubwa la bidhaa zinazotengenezwa na kiwanda hicho ni pamoja na kamba za plastiki ambazo husafirishwa China, Amerika, Urusi, Korea na Vietnam.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED