Kamati ya Bunge yabaini upigaji fedha maendeleo

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 10:32 AM Feb 05 2025
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatuma Toufiq.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatuma Toufiq.

KAMATI ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imebaini Sh. milioni 937.3 za Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) zilizokopeshwa hazijarejeshwa hali inayoathiri utoaji wa mikopo kwa wanawake kufikia tija iliyokusudiwa.

Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo jana bungeni, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatuma Toufiq, alisema mfuko huo ulianzishwa kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa mitaji ya uendeshaji wa miradi ya kiuchumi wanawake kwa kuwapa mikopo yenye masharti nafuu.

Alisema mfuko huo una mtaji wa kiasi cha Sh.bilioni 1.27  na kati ya fedha hizo zilizopo kwenye akaunti ni Sh.milioni 322. 5.

“Kiasi cha Sh. 475,488,459.90 ni madeni yalipo halmashauri ambayo hayajarejeshwa na Sh. 461,825,598 ni madeni ambayo wizara ilivikopesha vikundi vya wajasiriamali na mjasiriamali mmoja mmoja,”alisema.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, kamati imebaini kuwa kumekuwa na urejeshwaji usioridhisha kutoka halmashauri na vikundi vilivyokopeshwa hivyo kufanya mfuko kuwa na madeni ya muda mrefu na kupelekea kushindwa kutoa mikopo kwa walengwa.

“Kwa kuwa kumekuwa na mikopo ya muda mrefu iliyokopeshwa kwa halmashauri, wanawake na vikundi mbalimbali nchini na haijarejeshwa na kutorejeshwa kwa mikopo hiyo kunaathiri utolewaji wa mikopo kwa wanawake wengine wenye vigezo vya kupata mikopo hiyo na hivyo kuathiri nia njema ya serikali ya kuwainua wanawake kiuchumi,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema Bunge limeazimia serikali iweke mkakati unaotekelezeka wa kuhakikisha fedha zilizokopeshwa zinarejeshwa na kutumika kama ilivyokusudiwa.

Pia aliitaka serikali ibuni na kubainisha vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza mtaji wa mfuko na kuwanufaisha wanawake wengi zaidi.

Kuhusu ufanisi katika uratibu wa Mashirika Yasisyo ya Kiserikali (NGO), alisema kukosekana kwa rasilimali fedha na rasilimali watu kumesababisha kushindwa kufuatilia kwa kina mashirika takribani 9,773 yaliyoenea maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara na hivyo baadhi ya mashirika kujihusisha na shughuli ambazo ni kinyume na malengo ya usajili.

Alitaka serikali ichukue hatua za haraka na madhubuti ikiwa ni pamoja na kuyafuta mashirika ambayo yanajihusisha na masuala ya mmomonyoko wa maadili kinyume na tamaduni za nchi, yanayojihusisha na utakatishaji fedha pamoja na mashirika yanayojihusisha na siasa wakati wa uchaguzi.