DC Mhita aongoza kuanga miili miwili ya wachimbaji

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 03:24 PM Feb 05 2025
Wachimbaji wadogo wa mgodi wa Nkandi mbele ya masanduku a miili a wachimbaji wenzao waliofariki.
Picha:Shaban Njia
Wachimbaji wadogo wa mgodi wa Nkandi mbele ya masanduku a miili a wachimbaji wenzao waliofariki.

MKUU wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, ameongoza zoezi la kuopoa miili ya wachimbaji wawili kati ya watatu waliokuwa wamefukiwa na kifusi wakati wakichimba madini katika Mgodi wa Nkandi, Kata ya Zongomela, Manispaa ya Kahama.

Tukio hilo lilitokea Februari 1, mwaka huu, majira ya saa nne asubuhi katika duara namba saba. Baada ya siku tatu za jitihada za uokoaji, miili miwili ilipatikana huku mwili mmoja ukiwa bado haujapatikana. Miongoni mwa changamoto zilizokwamisha zoezi hilo ni kukatika kwa umeme na maji kujaa kwenye duara, hali iliyoathiri juhudi za kufanikisha uokoaji.

Mhita aliendesha zoezi hilo Februari 5, mwaka huu, katika viwanja vya Hospitali ya Manispaa ya Kahama, akishuhudiwa na viongozi mbalimbali. Alisisitiza kuwa hakuna wa kulaumiwa, kwani marehemu walipoteza maisha wakiwa katika harakati za kujitafutia riziki.

Alibainisha kuwa serikali imekuwa mstari wa mbele tangu siku ya kwanza ya tukio hilo, na itaendelea kuhakikisha mwili uliobaki unapatikana na kukabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za mazishi. Aidha, aliwataka wachimbaji kuchukua tahadhari wakati huu wa msimu wa mvua ili kuepuka ajali kama hizi. Pia, alilitaka Shirika la TANESCO kuhakikisha umeme haukwamishi juhudi za uokoaji wa mwili uliosalia.

Meneja wa Mgodi huo, Mdaki Shabani, aliwataja wachimbaji waliopoteza maisha kuwa ni Charles Zengo (23), mkazi wa Meatu, mkoani Simiyu, na Sule Hebi (24), mkazi wa Itilima. Alisema juhudi za kuupata mwili wa mchimbaji wa tatu zinaendelea, ingawa changamoto kubwa inasababishwa na kukatika kwa umeme mara kwa mara, hali inayopelekea maji kujaa kwenye duara na kusababisha ucheleweshaji wa zoezi la uokoaji.

“Leo tunawakabidhi miili hii kwa ndugu kwa ajili ya mazishi, huku tukizidi juhudi za kutafuta mwili wa mwisho. Changamoto kubwa ni kukatika kwa umeme mara kwa mara, hali inayotufanya kutumia muda mwingi katika kutoa maji badala ya kuendelea na uokoaji,” alisema Shabani.

Mmoja wa waombolezaji, Masanja Maige kutoka Itilima, aliipongeza serikali kwa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha miili miwili inapatikana licha ya changamoto za maji. Alitoa wito kwa serikali kushughulikia tatizo la umeme ili kurahisisha juhudi za kuupata mwili wa ndugu yao aliyesalia.