Watoto wawili wajiteka, wahojiwa na Kanda Maalum Dar

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 04:19 PM Feb 05 2025
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro
Picha: Mtan dao
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro

WATOTO wawili, miaka 16 na 12, wamehojiwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, baada ya kudaiwa kutoa taarifa za uongo za kutengeneza mazingira kuwa wametekwa na kwamba wanatakiwa fedha.

Kamanda wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro, amesema jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Anasema baada ya taarifa hiyo katika mahojiano ya kina, watoto hao ambao majina yao yanahifadhiwa, wamedai walifanya hivyo, ili kupata fedha kutoka kwa wazazi wao.

Kamanda anasema watoto hao mmoja ni mwanafunzi wa kidato cha pili na mwingine darasa la saba, wote ni wakazi wa Vijibweni Kigamboni, Dar es Salaam.

"Walitoweka Januari 26, mwaka huu, kuelekea Longoni Beach na walikesha huko hadi siku iliyofuata na baadaye walielekea Tungi hadi walipowapata wakizunguka Januari 29, mwaka huu ," anasema.

Kutokana na tukio hilo, Kamanda anasema Jeshi la Polisi, linalaani vitendo hivyo vya watu wenye lengo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.