RC Malima akabidhi mguu bandia aliyemwomba msaada

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 04:46 PM Feb 05 2025
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima akabidhi mguu bandia kwa Jackson Mwakalinga
Picha: Idda Mushi
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima akabidhi mguu bandia kwa Jackson Mwakalinga

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amekabidhi mguu bandia uliogharimu Sh. milioni 2.5 kwa Jackson Mwakalinga (75), mkazi wa Sangasanga, wilayani Mvomero, mwenye ulemavu.

Mguu huo bandia, umetengenezwa na Hospitali ya Jeshi ya Shirika la Mzinga na kuwasihi wahitaji wa huduma hiyo kufahamu kuanza kutolewa kwa huduma hiyo, mjini Morogoro.

Akikabidhi mguu huo bandia, Mkuu huyo wa Mkoa alisema aliguswa kumsaidia Mwakalinga, aliyekatwa mguu tangu mwaka 2006 na kukutana naye akipatiwa matibabu Agosti mwaka 2024, hospitali ya Mzinga.

Alisema alipokutana naye ilikuwa ni maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wakati huo hospitali ikitarajia kuanzisha kitengo cha viungo tuna na vifaa saidizi, kilichokamilika sasa.

Alisema JWTZ ni sehemu muhimu kwa mustakabali wa uhai wa taifa kwa namna nyingi na sio kwa ajili ya ulinzi pekee, bali pia ushiriki wa mfano kwenye masuala ya kijamii na kupongeza hatua ya hospitali Mzinga kuanza kutoa huduma ya viungo tiba na vifaa saidizi.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema Jackson, alimuomba amsaidie kupata mguu bandia na akaahidi kugharamia matengenezo yake na alielekeza uongozi wa Shirika hilo, kuanza kutoa huduma. "Kwa sasa wananchi wenye uhitaji wa huduma wa viungo bandia badala ya kukimbilia maeneo mengine ya mbali yenye huduma kama hizi.

“Ni vyema wakatumia uwekezaji huu uliofanywa na JWTZ katika kuboresha afya hasa ukizingatia mwaka 1976 hospitali hii, ilikuwa zahanati ya kutoa huduma kwa watu wachache, wakiwamo maofisa wa serikali na sasa ni kubwa kutoa huduma,” alisema Malima.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima akabidhi mguu bandia kwa Jackson Mwakalinga
Mwakalinga ambaye ni dereva wa zamani wa malori akisafiri nchi za nje, ikiwamo Burundi, alisema awali alichomwa na mfupa wenye ncha kali aliporejea nyumbani kwake, akitokea safarini.

"Kukatokea kidonda kisichopona, nyama za mguu zikawa zinaoza na kuanguka, nikaenda hospitali ya Taifa ya Muhimbili ndipo wakakata mguu wangu juu ya paja mwaka huo wa 2006,na sasa ni miaka 19 tangu kukatwa kwa mguu wangu.

“Nimehangaika makanisani na kila mahali kutafuta huduma ya mguu bandia bila mafanikio Hadi nilipopata msaada huu wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro," alisema Mwakalinga

Jackson Mwakalinga akabidhiwa mguu bandi
Meneja Mkuu wa Shirika la Mzinga na Mkuu wa Kikosi cha Jeshi Mazao, Brigedia Jenerali Seif Hamisi, alisema mguu huo, umetengenezwa kwa kiwango cha hali ya juu, kilichozingatia vigezo na viwango.

“Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob Nkunda aliagiza Malima kupunguziwa gharama kwa kufanyiwa Sh. milioni 2.1 kwa vile aliamua kumsaidia mhitaji.”

Brigedia Jenerali Hamisi, alisema hospitali ya Mzinga imeendelea kutoa huduma za matibabu ya kawaida na ya kibingwa ikiwemo magonjwa ya dharura, magonjwa ya wanawake magonjwa ya maambukizi kwa njia ya mkojo, mifupa, magonjwa ya ndani na sasa wameanza kutoa huduma hiyo mpya ya viungo tiba na vifaa saidizi.

Hospitali ya Mzinga inatajwa kuwa ni hospitali ya nne kutoa huduma za viungo na vifaa saidizi nchini.