DRC waitaka M23 kuondosha vikosi vyake Goma

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 05:45 PM Feb 05 2025
DRC waitaka M23 kuondosha vikosi vyake Goma.
Picha:Mtandao
DRC waitaka M23 kuondosha vikosi vyake Goma.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imetoa wito kwa vikosi vya waasi wa M23 vinavyotajwa kuungwa mkono na Jeshi la Rwanda, kuondoa askari wake katika mji wa Goma, mashariki mwa nchi hiyo.

Wito huo umetolewa leo, Februari 5, 2025, na Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Therese Kayikwamba Wagner, alipokuwa akizungumza na Shirika la Utangazaji la Newzroom Afrika la Afrika Kusini, kuhusu usitishaji vita wa upande mmoja uliotangazwa na waasi wa M23.

Wagner amesema kuwa serikali ya DRC inahitaji hatua za kweli na madhubuti kuthibitisha kuwa usitishaji vita huo si sehemu ya mkakati wa waasi kujihalalisha.

"Tunahitaji kuona hatua madhubuti, maana halisi ya hii ni kuwa na ushahidi kwamba hili si suluhisho la moja kwa moja," amesema Wagner.

Februari 3, 2025, kundi la M23 lilitangaza kusitisha mapigano baada ya wiki mbili za mapambano na jeshi la DRC, huku wakifanikiwa kuudhibiti mji wa Goma.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mapigano hayo yamesababisha zaidi ya watu 900 kuuawa na wengine 2,880 kujeruhiwa.

Wagner amesema kuwa kwa suluhu ya kibinadamu na kuruhusu misaada ya dharura kuingia Goma, ni lazima waasi waondoke kabisa katika mji huo.

"Lazima waasi waondoke mara moja ili Goma iwe huru na misaada ya kibinadamu iweze kuwafikia waathirika," amesisitiza Wagner.

Aidha, Waziri huyo wa Mambo ya Nje ameishutumu M23 na Jeshi la Rwanda kwa kukata huduma muhimu za maji, umeme, na kuzuia barabara zote zinazoingia na kutoka Goma.

Kwa upande wake, Msemaji wa Serikali ya DRC, Patrick Muyaya, amesema kuwa usitishaji vita wa waasi hao ni propaganda na kwamba wanachosubiri ni M23 kuondoka kabisa Goma.

"Hili ni porojo tu, hatutakubali. Tunachokitaka ni waasi waondoke Goma, hatutaacha mpaka tuurejeshe mji huu kwa namna yoyote," amesema Muyaya.

M23 imeendelea kukanusha tuhuma za kushirikiana na Rwanda, ikidai kuwa mapambano yao yanachochewa na madai ya ubaguzi dhidi ya jamii ya Watutsi katika eneo hilo.

Mzozo huu unaendelea kuzua taharuki kubwa, huku jumuiya ya kimataifa ikihimiza pande zote kutafuta suluhu ya kudumu kwa njia ya mazungumzo.