Ukwasi wa mawaziri, ma-RC wazua jambo

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 12:25 PM Dec 11 2024
Ukwasi wa mawaziri, ma-RC wazua jambo.
Picha:Christina Mwakangale
Ukwasi wa mawaziri, ma-RC wazua jambo.

UKWASI walionao baadhi ya mawaziri na wakuu wa mikoa na wilaya nchini umezua jambo: Watetezi wa haki za binadamu wamehoji walikopata ukwasi huo viongozi hao wa serikali.

Ni hoja iliyoibuliwa na watetezi hao jana jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa tafakuri ya hali ya utetezi na uenezi wa haki za binadamu nchini kwa kipindi cha miaka 40 ya uwapo wa haki hiyo kikatiba.  

Hao ni pamoja na Jenerali Ulimwengu, Askofu Emmaus Mwamakula, Shehe Ponda Issa Ponda, Mpale Mpoki, Tike Mwambipile, Hellen Kijo-Bisimba, Rugemeleza Nsala na Kaiza Buberwa. 

Bila kutaja jina la waziri, mkuu wa mkoa na wilaya, Ulimwengu, mwandishi mkongwe mwenye taaluma ya sheria, aliwataka waandishi wa habari wenzake wampatie majibu kuhusu ulikopatikana ukwasi walionao baadhi ya mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya nchini. 

"Ninyi waandishi wa habari, mmeshawahi kujiuliza mishahara ya viongozi -- mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya wanapata kiasi gani? Kile kipato chao halali! Masurufu anayopata yanayotokana na nini? Na akija madarakani, mali zake zinatokana na vyanzo gani? Au hii ni hela yetu ambayo ilipaswa kujenga barabara? 

"Au tunataka kuona anakula kwa kamba yake? Inawezekana kabisa nchi inashindwa kufanya shughuli zake... Nimewapa kazi hii waandishi wa habari. Mkishindwa, basi ninyi siyo waandishi wa habari. 

1

"Ninazungumza hivi, ninaomba mnisaidie vyombo vya habari, mimi nimeshastaafu," alisema Ulimwengu na kuibua kicheko ukumbini, huku akisisitiza ni umuhimu viongozi wa umma kutaja mali zao na kuwaruhusu waandishi wa habari kuona viapo vya kutangaza mali zao na kila mwaka waulizwe tena. 

Watetezi hao pia walionesha wasiwasi wao juu ya matukio yanayowakumba, huku wakitaka falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan kujengewa misingi ya kisheria ili itekelezeke. 

Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema falsafa hiyo ya Rais Samia ya Maridhiano, Ustahamilivu, Mageuzi na Kujenga Upya inaweza kuwa na nia njema ingawa changamoto ya utekelezaji wake iko katika mifumo na wanaomzunguka. 

"Falsafa ya Rais Samia inaweza kuwa yenye nia njema, shida ikawa kwa wanaomzunguka. Tumebaini hawana nia njema. Rais ndiye anataja haki za binadamu mara nyingi zaidi, haachi kila akizungumza, shida ni mifumo. Suala la Ngorogoro tulilizungumza bila woga, hatimaye akaunda tume," alisema. 

Olengurumwa alisema kuwa kwa miaka ya karibuni, kumekuwako woga wa utetezi na utekelezaji wa haki za binadamu kutokana na watetezi wengi, hasa wanazuoni, viongozi wa dini, wastaafu na waandishi wa habari kutokuwa thabiti kwenye utetezi, akitaja vikwazo kadhaa kama vile kuhofia usalama wao. 

2

"Awali wataalamu wa vyuo vikuu walielimisha na kutoa elimu, walionya. Ilichangia mabadiliko makubwa ya kisheria, yalianzia vyuo vikuu, waliona umuhimu wa utetezi wakiwa wadau wakuu.  

"Lakini hali inazidi kubadilika kadri siku zinavyozidi kwenda. Leo hii hali imebadilika, imeshuka! Huwezi kukuta mijadala, watu wakichambua, ukosoaji katika vyuo vya kitaaluma. 

"Unaweza ukaita mjadala pale Chuo Kikuu (UDSM), ukakuta wanaohudhuria siyo wanachuo, si wanafunzi! Hadhi ya chuo kikuu kuwa chemchemu ya mawazo imebadilika, kuna changamoto," alitadharisha. 

Kuhusu utetezi wa haki za binadamu kwenye mhimili wa mahakama, Olengurumwa alisema kuwa awali ulitumika kueneza na kutetea haki hizo kutokana na mamlaka iliyonayo. Sasa umeshuka kutokana na uamuzi unaotolewa hautekelezwi, akitolea mfano suala la mgombea binafsi ambalo halijatekelezwa na Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 ambayo Rebecca Gyumi alishinda kesi kuhusu umri wa kuoa na kuolewa. Nalo halijatekelezwa. 

Olengurumwa alitaja kundi lingine ni la viongozi wa dini ambao wao tangu historia na kwenye vitabu vya dini wamekuwa mstari wa mbele kwenye usawa wa binadamu pamoja na kuchangia huduma za kijamii kama vile ujenzi wa hospitali, shule na vyuo. 

 Alisema kuwa hivi sasa jamii na baadhi ya viongozi serikalini wanadhani utetezi wa haki kwa viongozi hao ni kukiuka miongozo ya kidini. 

Olengurumwa alisema kwamba kundi la mawakili limekuwa na mchango mkubwa kwa miongo minne nchini, lakini eneo la kisheria hivi sasa limepwaya. Wanakumbana na changamoto, huku baadhi wanaofika mahakamani wakionekana wasumbufu, hata kujengewa chuki na baadhi ya watoa uamuzi. 

3

“Mawakili wengi hawataki kujihusisha na haki za binadamu, ukiwa mtetezi unakuwa katika migogoro. Ulinzi ili ukamilike lazima kuwe na kundi kubwa la utetezi. Sehemu kubwa wanaotekwa ni wanaosemasema," alidai. 

Wakili Olengurumwa alisema kwamba kundi lingine la utetezi wa umma lililorudi nyuma ni la wazee wastaafu ambao ni wananchi waandamizi, akisema wanasita kukemea, kuonya na wakikaa kimya kwa kujifungia na maarifa, uzoefu na familia zao.

 "Huu ni uchoyo wa maarifa na hekima. Viongozi waliobaki wachache ndio wanasema. Tumemsikia Jaji Warioba, Butiku na wengine wanajitokeza kusema kusaidia watanzania," alisema Olengurumwa. 

Alisema asasi za kiraia awali zilifanya kazi kwa nyakati ngumu na kusikika nchi nzima. Hakukuwa na teknolojia ya mawasiliano, lakini hivi sasa watetezi hao wamerudi nyuma kuusemea na kuutetea umma, hata kwenye masuala ya uchaguzi. 

"Suala la utekaji limechagiza watetezi wa haki za binadamu kwa makundi yote - mawakili, waandishi wa habari kurudi nyuma. Kwa mwaka mmoja waliotekwa kwa takwimu zetu ni watu 47 ingawa Jeshi la Polisi wao wanatoa takwimu za watoto kupotea.

 "Takwimu za watu wazima ni chache na wakitaja wanatamka watu wamepotea, si kutekwa! Wamebadili lugha. Tangu mwaka 2016, watu waliotekwa ni zaidi ya 250," alidai. 

Pia alisema kwamba kundi la waandishi wa habari ambalo ni la utetezi kwenye haki za binadamu nalo limekwamishwa na sheria ambazo zinawawabana, kwa kuminya uhuru wa habari, huku hadhi ya sekta hiyo ikishuka. 

"Waandishi wa habari wengi sasa ni habari za kusifiasifia, hiyo ni mbaya! Matukio mengi mnafumbia macho, ingawa ni hatari, ila kunahitajika mbinu za kujikomboa bila kubagua. Kwa watetezi hawa karibu wote niliowataja, kunahitaja uhuru wa kiuchumi ili kutimiza majukumu ambayo ndio utetezi wenyewe," alieleza Olengurumwa. 

4

SIMBA NA YANGA

Naye Ulimwengu alisema licha ya kuwapo mambo ya msingi ya kujenga hoja za kuikwamua nchi, vyombo vya habari nchini vimejawa mijadala inayoegemea burudani na michezo, hasa soka, wakizungumzia zaidi mwenendo wa timu za Simba na Yanga.

 Alisema mijadala hiyo ingekuwa na uzito iwapo hata soka la taifa lingekuwa linafanya vyema, kitaifa na kimataifa, hivyo vyombo vya habari, hasa vya umma, viweke kipaumbele katika kujenga hoja za msingi, ikiwamo utetezi wa haki za binadamu. 

"Yaani katika vyombo vya habari vya umma, binafsi kumejawa na ‘usimba na uyanga kutwa nzima’. Wajibu wa waandishi wa habari uko wapi? Sisemi ni mbaya, ila isivyo bahati, hata huo mpira wenyewe hatuujui," alionya. 

Naye Askofu Mwamakula alisema jamii inatakiwa kubadili dhana kwamba viongozi wa dini ni watetezi wa haki za binadamu, hivyo wanapokuwa mstari wa mbele kuzitetea, wasione ni ukiukwaji miongozo ya dini. 

"Kama unafuata amri 10 za Mungu, ujue wewe ni mtetezi wa haki za binadamu. Ilipoanza serikali kuminya haki za kisiasa na viongozi wa dini wakaanza kutetea, ikaanza kuonekana wanapingana na serikali. Changamoto zikaanza katika mazingira hayo, wako wanaotishiwa kufutiwa usajili," alidai Askofu Mwamakula. 

5

Mwanaharakati wa Haki za Binadamu, Helen Kijo-Bisimba, alisema utetezi wa haki za binadamu nchini umeendelea kuzorota, hasa kwa asasi za kiraia, jambo linalochangia kutoimarika kwa utetezi huo. 

Naye Shehe Ponda alikosoa Sheria ya Ugaidi kwamba ina vifungu vinavyomruhusu askari kumhoji na kumtesa mshtakiwa/ mtuhumiwa, akisema hatua hiyo inarudisha nyuma utetezi wa haki za binadamu. Mtu anaadhibiwa hata kabla hayajapatikana na hatia. 

Wakili Dk. Nshala alisema kwamba hivi sasa wanazuoni wamepungua nguvu ya utetezi wa haki za binadamu kwa kuwa walio wengi wanaangalia maslahi binafsi, ikizingatiwa mtoa ajira wa kundi hilo vyuoni ni serikali, hivyo utoaji hoja unaokosoa serikali huwa ni mgumu kwao.

6