Watoto njiti wakumbukwa hospitali ya Mkoa wa Shinyanga

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 09:34 PM Dec 12 2024
Jaji wa Mahakama kuu Kanda ya shinyanga Ruth Massam (kulia) akimkabidhi mashime ya kupumulia  watoto Njiti, kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dk.Luzila John.
Picha:Marco Maduhu
Jaji wa Mahakama kuu Kanda ya shinyanga Ruth Massam (kulia) akimkabidhi mashime ya kupumulia watoto Njiti, kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dk.Luzila John.

Timu ya wanasheria wanawake Mkoa wa Shinyanga, ikijumuisha majaji, mahakimu, wanasheria wa serikali, na mawakili wa kujitegemea, imekabidhi zawadi mbalimbali kwa watoto njiti waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Zawadi hizo ni pamoja na mashine ya kusaidia kupumua.

Hafla hiyo ilifanyika jana kama sehemu ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu kuelekea kufunga mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2025.

Kiongozi wa timu hiyo, Jaji Ruth Massam wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, alisema lengo la ziara yao lilikuwa kusaidia watoto njiti kwa kuwapatia vifaa muhimu.

"Tumetoa zawadi zikiwemo kanga, soksi, shuka, na mashine ya kusaidia kupumua, vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni nne," alisema Jaji Massam.

Pia, Jaji Massam alitoa wito kwa mashirika na taasisi mbalimbali kutembelea hospitali hiyo na kutoa msaada kwa watoto njiti ili kusaidia kuokoa maisha yao.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Luzila John, alishukuru timu hiyo kwa msaada waliotoa na kuhimiza ziara za aina hiyo kuendelea.

"Mashine hii ya kusaidia kupumua itakuwa msaada mkubwa kwa watoto njiti. Pia, tunapokea kwa mikono miwili zawadi hizi na moyo wa faraja ambao mmeonyesha kwa wagonjwa wetu," alisema Dk. Luzila.