WATAALAM wa afya ya kinywa na meno kutoka nchi za Afrika Mashariki wametakiwa kuacha matumizi ya dawa yenye zebaki inayotumika kuziba meno, kwani ina madhara makubwa kwa afya ya watoto, wanawake wajawazito, na mazingira.
Wito huu umetolewa kama sehemu ya maadhimisho ya Afrika ya kuziba meno bila kutumia dawa yenye zebaki, yaliyopitishwa miaka 10 iliyopita na asasi za kiraia zipatazo 40 katika mkutano wa kimataifa uliofanyika jijini Abuja, Nigeria.
Maadhimisho haya ya kila mwaka yanaadhimishwa kuanzia tarehe 9 hadi 14 Desemba, huku lengo kuu likiwa ni kutambua na kuhimiza utekelezaji wa Mkataba wa Minamata wa Zebaki, ambao unazitaka nchi wanachama kutekeleza mabadiliko ya kisheria kuhusu matumizi ya zebaki. Kauli mbiu ya mwaka huu inasema: “Nchi wanachama wa Mkataba wa Minamata wa Zebaki watekeleze matakwa ya mkataba huo.”
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam jana Dorah Swai, Katibu Mtendaji wa Asasi ya AGENDA for Environment and Responsible Development (AGENDA) iliyoko Dar es Salaam, alisema kuwa matumizi ya Dental Amalgam (dawa ya kuziba meno yenye zebaki) yanahusisha madhara makubwa kwa afya, hususan kwa watoto chini ya miaka 15, wanawake wajawazito, na wanawake wanaonyonyesha.Dawa hii ina zebaki kwa asilimia 50, na inatakiwa kuepukwa kabisa kwa makundi haya kutokana na madhara yake kwa ubongo wa mtoto, ambayo yanaweza kuathiri ukuaji wake na uwezo wake wa kufikiri.
Silvani Mng’anya, Afisa Programu Mkuu wa AGENDA, analisema zebaki ina uwezo wa kuathiri afya ya mtoto tangu akiwa tumboni kwa mama, na kupitia maziwa ya mama wakati wa kunyonyesha. Hii inasababisha athari kubwa kwa maendeleo ya kiuchumi ya mtoto pindi atakapokuwa mkubwa. Aidha, zebaki huchukua muda mrefu kudumu katika mazingira, na kwa kupitia samaki, inaweza kuingia mwilini mwa binadamu, hivyo kusababisha madhara ya kiafya.
Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinatakiwa kuchukua hatua ili kuhakikisha dawa za kuziba meno zinazotumika hazina zebaki. Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizochukua hatua na kuzuia matumizi ya dawa yenye zebaki tangu mwaka 2022.
Bernard Kihiyo, Mkurugenzi wa Asasi ya Tanzania Consumer Advocacy and Research (TCAR), alisisitiza kuwa ni muhimu kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki kutumia dawa zisizo na zebaki ili kulinda afya ya watoto na mazingira, na kutimiza haki za watoto katika kanda hii. Alisema kwamba matumizi ya dawa salama ni muhimu kwa mustakabali bora wa watoto na jamii kwa ujumla.
Mkataba wa Minamata wa Zebaki, uliopitishwa mwaka 2013 nchini Japan, unatoa mwongozo wa kimataifa kuhusu jinsi ya kukomesha matumizi ya zebaki katika bidhaa na maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na dawa ya kuziba meno. Hadi sasa, nchi 151 zimeidhinisha mkataba huu, na unalenga kulinda afya za watu na mazingira dhidi ya madhara yanayotokana na zebaki.
Kwa kufanya hivyo, nchi hizo zinapata fursa ya kuondoa madhara makubwa ya zebaki na kuhakikisha kuwa afya ya watoto na wanawake wanavyonyonyesha, pamoja na mazingira, vinakuwa salama kwa vizazi vijavyo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED