MKUU wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi, amewaasa wananchi wa Wilaya ya Ileje kuungana na kushirikiana kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia, kukemea na kushirikiana na vyombo vya dola kutoa taarifa ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ili jamii iwe salama.
Akizungumza mapema juzi wakati wa kilele cha maadhimisho ya Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia wilayani humo, ambapo alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, ametoa wito kwa wananchi kubadilika na kuachana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Amesema vitendo hivyo vinarudisha nyuma ustawi wa jamii na kuzorotesha uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Aidha, amewasihi wazazi kuwalinda watoto kwa kuwapa malezi stahiki yanayozingatia maadili ya Kitanzania ili kuwaepusha watoto kuiga tamaduni za nje ambazo zinakiuka miiko ya maadili ya nchi yetu.
Katika hatua nyingine, mkuu wa wilaya huyo aliziasa familia kudumisha upendo na kuepuka migogoro sambamba na kutumia fursa zilizopo katika wilaya kujiongezea kipato kitakachowasaidia kutunza na kulea familia.
Aidha, Mgomi alitoa rai kwa Jeshi la Polisi kupitia dawati la jinsia kuendelea kushirikiana na wananchi kwa kutoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia sambamba na kuchukua hatua stahiki kwa wale wole watakaokutwa na hatia ya kujihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED