Maafisa usafirishaji wa Manispaa ya Shinyanga wamepewa elimu kuhusu uzingatiaji wa sheria za usalama barabarani ili kudhibiti ajali zinazoongezeka mwishoni mwa mwaka na wakati wa kuukaribisha mwaka mpya.
Aidha, wameonywa kuacha tabia ya kubebesha wanafunzi kwenye mapaja ya abiria wanaume.
Elimu hiyo ilitolewa Desemba 12, 2024, na Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Umma kutoka Trafiki Makao Makuu, ACP Michael Deleli Stephen, katika ukumbi wa Bwalo la Polisi, Manispaa ya Shinyanga.
ACP Stephen amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi linafahamu umuhimu wa maafisa usafirishaji na limekuwa likitoa elimu mara kwa mara kuwakumbusha wajibu wao wa kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazotokana na uzembe wa madereva.
“Tunaelekea kufunga mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka mpya 2025. Ni muhimu maafisa usafirishaji wawe makini na matumizi salama ya barabara ili kumaliza mwaka salama,” amesema ACP Stephen.
Aidha,ametaja mambo ambayo madereva hao ambayo wanapaswa kuzingatia ili kutii sheria za usalama barabarani, kuwa ni wavae kofia ngumu,kutoendesha mwendokasi,kuzidisha abiria, na ku-“ovetake” hovyo,pia amewasisitiza wawe wana vaa sare,kuwa na lessen pamoja na vyombo vyao kuvikatia bima.
Aidha, amewakumbusha maafisa hao kuepuka vitendo vya ukatili wa kijinsia, kama kushika maungo ya wanawake kiholela, kutongoza wake za watu, au kufanya vitendo visivyofaa wanapopeleka huduma za nyumbani.
Kaimu Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Shinyanga, SP Methew Ntakije, ameonya madereva wa bodaboda dhidi ya matumizi mabaya ya kofia ngumu, kama kuweka kofia hizo chini ya miguu badala ya kuzivaa kichwani. Alisema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka.
Naye Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Shinyanga, ACP Fraterine Tesha, amewataka maafisa usafirishaji kushirikiana na Askari Kata kuripoti matukio ya uhalifu.
Maafisa usafirishaji wametoa shukrani kwa kupatiwa elimu hiyo na kuahidi kufuata sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali, hasa katika msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED