TPA, DP World zawatega wafanyakazi wa bandari

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:31 PM Mar 23 2024
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa.
PICHA: TPA
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa.

MAMLAKA Ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imetoa tangazo kwa watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam likiwataka kuchagua ama kubaki katika ajira TPA au kusitisha mikataba na kujiunga na ajira mpya katika kampuni ya DP World.

Taarifa ya TPA iliyotolewa Machi 20, mwaka huu, na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, imesema Oktoba 22, 2023, mamlaka hiyo iliingia mkataba na Kampuni ya DP World ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuhusu uendeshaji wa gati namba sifuri hadi namba tatu na gati namba nne hadi namba saba za Bandari ya Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka 30.

“Kutokana na makubaliano hayo yanayohusisha usimamizi na uendeshaji wa maeneo tajwa, watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam wanapaswa kuchagua kati ya kubaki TPA au kusitisha mkataba wa ajira kati yao na  TPA au kusitisha mkataba wa ajira wa TPA na papo hapo kuajiriwa upya na kampuni ya DP World,” imesema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uongozi wa TPA umekamilisha mchakato wa utoaji wa elimu kwa watumishi wote walio kwenye maeneo husika.

Taarifa pia imesema mchakato wa utoaji elimu ulianza Machi 4 hadi 19, mwaka huu, kwa lengo la kuwapa watumishi wote uelewa sahihi wa mabadiliko ya uendeshaji yanayoendelea katika Bandari ya Dar es Salaam.

“Pamoja na masuala mengine, elimu hii inahusisha mabadiliko ya uendeshaji wa bandari, utaratibu wa makabidhiano, utaratibu wa mtumishi kusitisha mkataba na TPA na papo hapo kuajiriwa upya na kampuni ya DP World kwa  mtumishi atakayekuwa ameamua kufanya hivyo kwa hiari yake mwenyewe bila kushurutishwa.

“Pia kuna stahiki ambazo zitatolewa na TPA kwa mtumishi atakayeamua kusitisha mkataba wa ajira wa TPA na kuajiriwa upya na Kampuni ya DP World,”.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kwa msingi huo, watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam wanajulishwa kuwa makabidhiano kati ya TPA na DP World yameanza kutekelezwa kwa kuwa, mchakato wa utoaji elimu kwa watumishi umekamilika.

“Watumishi watakaoamua kuajiriwa upya na kampuni ya DP World wanatakiwa kufika na kuorodhesha taarifa zao jengo la TPA Makao Makuu ukumbi wa mikutano ghorofa ya 32 kabla au ifikapo Machi 29, mwaka huu,” imesema.