BODI ya Chai Tanzania (TBT), imekutana na wadau wa zao hilo nchini kwa lengo la kujadili namna ya kukabiliana na changamoto zinazo wakwamisha.
Baadhi ya changamoto zilizotajwa kukwamisha ni pamoja na kukatika kwa umeme, ubovu wa miundombinu ikiwamo barabara.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Kaimu Mkurugenzi Bodi hiyo, Beatrice Banzi alipokutana na wadau kutoka serikalini, TBT, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), bandari, maofisa kutoka vyama vya ushirika na Wizara ya Kilimo kwa lengo kuangalia namna ya kutatua changamoto hizo.
“Pia tutajadili namna ya kuongeza ubora wa chai ili kulishika soko la chai ndani na nje ya nchi, lakini pia tutafanya hamasa kwa Watanzania wanywe chai kwa wingi na hasa inayozalishwa nchini kwa sababu inaonekana unywaji chai upo chini," alisema Beatrice.
Aidha, alisisitiza lengo lao lingine ni kupanga kwa pamoja ili kufikia malengo waliojiwekea kuendeleza zao hilo kwa muda wa miaka 10 kuanzia mwaka 2024 mpaka 2034.
“Lakini ili kufikia malengo hayo, lazima watu wa serikali, sekta binafsi wakae chini kwa pamoja kujadili ni jinsi gani wanaweza kuokoa zao hilo,” alisema na kuongeza:
“Hapa ni kama tunafanya ‘road map’ ili tuweze kujua tunaendaje, kama ni kuongeza uzalishaji wale wadau wanaohusika na uzalishaji tunapanga kwa pamoja tunafanyaje”.
Vilevile alisema: “Kama tunataka kutangaza chai yetu ndani na nje ya nchi tunafanyaje kwa kushirikiana na TANTRADE kwa hiyo yale majadiliano yetu sisi washiriki wa mkutano wa leo ndiyo yatatumika kama ‘road map’ yakuweza kuboresha huu mkakati ambao tumeupanga kuinua na kuendeleza zao la chai kwa hiyo miaka kumi”.
Aidha, alisema katika kikao hicho watatambulisha nembo ya chai ya Tanzania ili iwe rahisi kutambuliwa hata ikiuzwa nje ya nchi na kwamba wanaamini hatua hiyo itasaidia kukuza biashara ya zao hilo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED