Nyagango aibuka kinara wahitimu PhD ya MoCU

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 02:24 PM Dec 12 2024
Nyagango aibuka kinara wahitimu PhD ya MoCU
Picha:Mpigapicha Wetu
Nyagango aibuka kinara wahitimu PhD ya MoCU

ALEX Nyagango, ambaye ni miongoni mwa wahitimu sita wa Shahada ya Udaktari wa Falsafa (PhD) katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, ameibuka kuwa mshindi wa jumla katikati ya wanazuoni waliofanya vizuri zaidi kwenye masomo na kupata tuzo ya Sh.700,000.

Tuzo hiyo inayotolewa na Makamu Mkuu wa Chuo (MoCU), inalenga kuchochea matokeo chanya katika masomo na shughuli za ubobezi katika mitaala.

Nyagango, alitangazwa jana na kukabidhiwa tuzo hiyo leo na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi nchini (PSPTB), Godfred Mbanyi, wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo (prize giving ceremony) katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).

Hafla hiyo iliambatana pia na majilisi yaliyowahusisha wasomi na wanazuoni waliowahi kusoma MoCU na miaka 10 ya chuo hicho.

Nyagango, aliwazidi wenzake waliohitimu PhD, ambao ni Bernadette Temba, Emmanuel Mkilia, George Budotela, Julieth Koshuma na Pamela Liana.

Kabla ya kukabidhi tuzo hizo, Makamu Mkuu wa Chuo MoCU, Prof. Alfred Sife, amesema mwaka huu, chuo hicho kinaadhimisha miaka 10 tangu kupewa ithibati ya kuwa chuo kikuu kamili mwaka 2014.

Kwa mujibu wa Prof. Sife, tuzo hiyo mbali na mhitimu huyo wa PhD, imewahusisha wahitimu wa fani mbalimbali 102, ambapo kati yao wanaume ni 74 na wanawake 28.