Itakumbukwa kwamba mwezi machi 30, 2024 jijini Bujumbura nchini Burundi, Waziri wa Madini Tanzania Anthony Mavunde na Waziri wa Maji, Nishati na Madini nchini Burundi Mhandisi Ibrahim Uwizeye kwa pamoja walisaini Hati ya Makubaliano (MoU) kuhusu Ushirikiano wa kikazi katika Sekta ya Madini kupitia mikakati mbalimbali ya kisekta ili kuendeleza uchumi wa nchi zote mbili.
Katika kutekeleza mashirikiano hayo , mnamo Desemba 11, 2024 Ujumbe maalum kutoka Serikali ya Burundi ulifika Tanzania na kukutana na uongozi na wataalam wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ukiwa na lengo la kujifunza kuhusu maendeleo ya Sekta ya Madini katika mnyororo wa thamani madini hususan katika vipengere vya Uongezaji thamani madini, tafiti za kina , namna bora ya kusimamia Sheria na taratibu za biashara ya madini.
Kwa mujibu wa MoU, Tanzani ikiwa na uzoefu wa muda mrefu katika Sekta ya Madini itatoa Utalaam wake nchi ya Burundi katika kuimarisha taratibu za uchimbaji salama na endelevu.
Aidha, itatoa mafunzo na kugawana maarifa kuhusu teknolojia ya kisasa na kuanzisha miradi ya pamoja ya utafiti wa madini ambapo kwasasa Burundi inatafuta kuboresha miundombinu na teknolojia ya uchimbaji.
Sambamba na hapo, pande zote mbili zitajadiliana kuhusu ujenzi wa viwanda vya uchakataji, uchenjuaji na usafishaji madini pamoja na kujengeana uwezo kwa taasisi na wataalam wa pande zote.
Ujumbe huo umeongozwa na Niyongabo Regis ambaye ni mshauri wa masuala ya madini kutoka Wizara ya Maji , Nishati na madini nchini Burundi.
Pamoja na mambo mengine , ujumbe huo utapata fursa ya kujifunza hatua za maendeleo ya sekta ya madini kupitia taasisi tendaji zilizochini ya Wizara ya Madini ambazo ni taasisi ya GST, STAMICO,Tume ya Madini,TEIT na TGC.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED