Mwinyi aagiza timu Dira Maendeleo 2050 kukusanya maoni kwa wadau

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 02:16 PM Dec 12 2024

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha:Mpigapicha Wetu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameiagiza timu kuu ya kitaalamu ya Dira ya Maendeleo ya 2050 kukutana na wadau mbalimbali kuhakikisha kazi ya kupokea maoni inakamilika kikamilifu ili kuwa na dira yenye kubeba maono ya wananchi wote.

Pia Dk. Mwinyi ameziagiza Tume za Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Serikali ya Mapiduzi ya Zanzibar kuhakikisha wanaratibu zoezi la uhakiki kwamba linafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu pamoja na kuisambaza rasimu hiyo kwa vyombo mbalimbali na kuweka mfumo halisi wa kupokea maoni.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo visiwani hapa alipozindua Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali za SMT na SMZ akiwamo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi amewaagiza viongozi na wataalamu wote wa serikali zote mbili kutoa ushirikiano kwa timu ya kitaalamu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuwa kutoshiriki kwao hakutofanikisha azma ya dira hiyo.

Alisisitiza timu hiyo ya kitaalamu inamfikia kila mwananchi nchini ili kutoa maoni bila kujali tofauti za dini, siasa, jinsia, makundi maalum au eneo mtu analotoka ili ibebe maono yao ya miaka 25 ijayo.

Alisema malengo makuu ya rasimu hiyo ni kuona yamegusa moja kwa moja katika kuboresha maisha ya watu, elimu, afya, ustawi wa amani na haki pamoja na kuwa na dira jumuishi ambayo itamshirikisha kila mwananchi kutoa mchango wake kwa maendeleo ya taifa.

Aliishauri timu hiyo kuweka muktadha wa maendeleo ya taifa katika mwelekeo wa makubaliano au mipango ya kikanda na kimataifa, akitoa mfano “Dira ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki” (EAC) 2050; “Dira ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika” (SADC) 2050; “Makubaliano ya Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi” (Paris Agreement); “Ajenda ya Maendeleo ya Afrika” (Ajenda 2063); “Doha Programme of Action 2022 – 2023” na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs).

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliishauri timu hiyo ya kitaalamu kuandaa usimamizi mzuri wa kukusanya maoni ya wadau kwa kuzunguka nchi nzima na kuandaa makongamano na majadiliano na wadau.

Akitaja mafanikio ya Dira ya 2025 ambayo inafikia tamati mwezi Juni 2025, alisema kuwa ni pamoja na kuboresha hali ya maisha ya watu, elimu, uboreshaji wa huduma za afya, kupunguza vifo na kuongezeka wastani wa umri wa kuishi, kuimarika kwa utawala wa kisheria na ukuaji wa uchumi.

Alisema, kwa kipindi chote cha utekelezaji wa Dira 2025, nchi imekuwa kitovu cha amani na imeshiriki kikamilifu hata katika duru za kimataifa kulinda amani barani Afrika, aliwasisitiza Watanzania kuendelea kulinda amani, utulivu na umoja kama misingi muhimu ya kupata maendeleo ya nchi.

Alisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zenye utoshelevu wa chakula kwa asilimia 124, licha ya kuwa bado kilimo hakijawa cha kisasa, lakini wakulima wamefanya kazi kubwa ya kuhakikisha nchi haikabiliwi na njaa. 

Akizungumzia ustawi wa elimu alisema kumeshuhudiwa ongezeko kubwa la madarasa, vyuo vikuu na walimu, aidha, udahili wa elimu ya msingi umeongezeka kutoka asilimia 69 kutoka mwaka 2000 hadi kufikia asilimia 97 mwaka 2022, kuongezeka kwa kiwango cha kumaliza elimu kutoka asilimia 51 mwaka 2000 hadi asilimia 70 mwaka 2022 na kufanikiwa kuondoa pengo kubwa lililokuwapo katika elimu ya msingi na sekondari kati ya watoto wa kike na watoto wa kiume. 

Kuhusu uboreshaji wa huduma za afya alisema Dira 2025 ilifanikiwa kupunguza vifo na kuongezeka wastani wa umri wa kuishi, kuimarika kwa hizo kuanzia kwenye vituo vya fya, zahanati, hospitali za wilaya, mikoa, kanda hadi taifa.

Akielezea utawala bora na utawala wa sheria ameeleza kuwa limebaki kuwa kipaumbele kwa taifa licha ya changamoto ndogo ndogo ambazo zimeendelea kushughulikiwa na serikali kwa masilahi mapana ya wananchi ikiwamo kuundwa kwa Tume ili kupendekeza namna ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini ikiwa ni njia ya kuendelea kuimarisha zaidi mifumo ya haki jinai na hivyo kudumisha utawala bora na utawala wa sheria. 

Kuhusu uchumi alisema umekuwa kwa wastani wa asilimia 6.7 ikiwamo kukua kwa biashara na uwekezaji, kujenga miundombinu muhimu kwa sekta zote ujenzi wa barabara na madaraja makubwa, reli ya kisasa, ukarabati mkubwa wa reli ya kati, bandari, meli, viwanja vya ndege, miundombinu ya mkongo wa taifa wa mawasiliano. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema uzinduzi wa rasimu ya 2050 ni jambo kubwa lenye mustakabali muhimu kwa Taifa la Tanzania.

Alisema kuwa rasimu hiyo ni ya Watanzania wote na kuahidi timu ya kitaalamu ya dira hiyo kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uaminifu ili hatimaye kuwa na Dira ya 2050 yenye tija na manufaa kwa Watanzania.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–Mipango na Uwekezaji ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Kitaifa ya Maandalizi ya Dira 2050, Prof. Kitila Mkumbo, alisema msingi mkuu wa rasimu hiyo umejikita katika usalama, amani na utulivu na kuwa na uchumi imara.

Dk. Saada Mkuya Salum, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango na Makamu Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Uongozi ya Kitaifa ya Maandalizi ya Dira 2050, alisema Zanzibar imeshiriki kikamilifu kutoa maoni juu ya rasimu hiyo kwa hatua mbalimbali ikiwamo kuratibu maoni ya wananchi huku kukiwa na ushiriki mkubwa wa wanawake. 

Rais Dk. Mwinyi alikabidhi Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaliwa kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na watendaji wakuu wa taasisi za umma na binafsi.