WATU 200 wamepatiwa huduma ya kuwekewa puto kwenye tumbo la chakula, ili kudhibiti uzito uliokithiri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi, ameyasema hayo leo, jijini Dar es Salaam, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma za MNH na tathmini ya mwaka 2024.
Huduma ya kuweka puto ilianzishwa na MNH-Mloganzila, Desemba mwaka 2022, maalumu kupunguza nafasi kwenye tumbo la chakula hivyo kusababisha mtu kula kidogo.
Mara kadhaa, Prof. Janabi amesema visababishi vikuu vilivyothibitika kuchangia viharusi ni pamoja na uzito. Kuweka puto (intragastric Balloon) ni teknolojia mpya ya uhakika ya kusaidia wagonjwa kupunguza uzito.
Teknolojia hiyo ilipata idhini ya Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (Federal Food and Drags Authority -FDA) mwaka 2015. Mamlaka hiyo ndiyo inayoidhinisha matumizi ya mifumo mipya ya matibabu duniani.
Utaratibu wa kuweka puto tumboni hautumii upasuaji, Bali huingizwa kupitia mdomoni hadi tumboni. Wanaofaa kufanyiwa utaratibu ni wale wagonjwa wenye uzito uliopitiliza, yaani wenye uzito kuanzia kilo 90 kwenda juu au wale ambao kwa kipimo cha BMI cha zaidi ya 31.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED