Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imezindua Kampeni ya Shangwa la Sikukuu na TANAPA leo Desemba 13, 2024 jijini Arusha lengo likiwa ni kuhamasisha Watanzania na wasio Watanzania kutembelea Hifadhi za Taifa kipindi hiki cha msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya 2025.
Akizingumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Jully Bede Lyimo anayeshughulia Maendeleo ya Biashara TANAPA amesema, “TANAPA tuna hifadhi za Taifa 21 ambazo ni miongoni mwa Hifadhi Bora Afrika na Dunia kwa ujumla na zipo karibu kila mkoa wa Tanzania. Hivyo ushiriki wa watanzania kuzitembelea mbali na kufurahia uasili pia mtazitangaza.
Aidha, Kamishna Lyimo ameongeza kuwa fedha za viingilio wanazotoa watanzania hao huchangia katika kuongeza pato la Taifa ambalo huenda moja kwa kwenye ujenzi wa miundombinu ya barabara, Viwanja vya ndege, ujenzi wa Hospitali na mashule.
Kwa zaidi ya miongo sita tangu kuanzishwa kwake, TANAPA imeendesha kampeni nyingi lengo likiwa ni kuhamasisha Watanzania kujiwekea utaratibu wa kutembelea vivutio vya utalii vinavyopatikana ndani ya hifadhi hizo.
Kwa mwaka huu kampeni hii ya Shangwe la Sikukuu na TANAPA inalenga kupita ofisi moja baada ya nyingine, mtaa kwa mtaa, mlango kwa mlango kuhakikisha watanzania wengi wanahamasika kutembelea Hifadhi za Taifa Tanzania.
Uzinduzi wa Kampeni hii umeanza kwa maandamano ya matembezi ya miguu yaliyochukua takribani saa 3 kupita katika viunga mbalimbali vya jiji la Arusha na kuishia viwanja vya Gymkhana ikiwahusisha TANAPA, Chuo cha Utalii cha Taifa, wadau mbalimbali wa utalii, Mchekeshaji Eliud Samwel, Waandishi wa Habari na wananchi mbalimbali.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED