LICHA ya kupoteza pointi tatu mbele ya Azam FC juzi katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ameweka pembeni kipigo hicho na sasa jicho lake lipo katika mechi ijayo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Katika mchezo huo wa juzi, Azam FC ilishinda mabao 2-1, huku lile la ushindi likiwekwa nyavuni na kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’, dakika ya 51, na baada ya hapo akawaomba radhi mashabiki wa timu hiyo.
Hata hivyo, Yanga ilipata pigo kuelekea mechi dhidi ya Mamelodi itakayopigwa Machi 30, mwaka huu, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, baada ya winga wao, Pacome Zouzoua na beki wa kulia, Kouassi Attohoula Yao, kupata majeraha na kushindwa kuendelea na mchezo.
Baada ya kukamilika kwa mchezo huo, Gamondi amesema mechi ilikuwa ya ushindani mkubwa na amewapoteza wachezaji wake wawili.
"Tumeongeza wachezaji majeruhi baada ya kulazimika kumtoa Pacome na Attohoula Yao ambao waliumia.
"Wachezaji hao wako chini ya uangalizi na bado hatujapata taarifa juu ya majeraha yao, tumepoteza mechi na tunarejea katika uwanja wetu wa mazoezi kuangalia tulipokosea,” amesema kocha huyo.
Kuhusu hali ya kiungo wao, Khalid Aucho, Gamondi amesema nyota huyo anaendelea vizuri na matarajio yake ni kuonekana katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns.
Amesema Aucho anaendelea vizuri na ameshaanza mazoezi mapesi akiwa gym chini ya uangalizi na baada ya muda mfupi atarejea uwanjani kufanya mazoezi ya ushindani na mechi ya kimataifa anaweza kuwa sehemu ya kikosi.
“Natarajia Aucho atakuwa sehemu ya kikosi katika mchezo wetu ujao, kwa sababu tayari ameshaanza mazoezi mepesi, lakini tunasubiri taarifa kutoka kwa daktari juu ya asilimia ya kupona kwake na kuweza kucheza mechi hiyo ya ushindani,” amesema Gamondi.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo dhidi ya Mamelodi, amesema amewapa mapumziko mafupi wachezaji wake kwa sababu tangu walipomaliza mechi ya hatua ya makundi dhidi ya Al Ahly hawajapata muda wa kupumzika.
Gamondi alisema baada ya mapumziko mafupi watarejea uwanjani kujiandaa na mchezo dhidi ya Mamelodi ambao ni timu yake ya zamani ambayo aliwahi kuifundisha.
Kuhusu mchezo dhidi ya Azam, Gamondi amesema walifanya makosa katika boksi lao na Azam FC kufanikiwa kusawazisha na kipindi cha pili kutumia nafasi waliyoitengeneza kufunga bao la pili ambalo alidai halikuwa sahihi kwa kuwa lilikuwa la kuotea 'offside'.
“Bao la pili halikuwa sahihi, mfungaji aliotea ‘Offside’, waamuzi hili hawajaliona, lakini ndio mpira ulivyo," amesema.
Kwa upande wa Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema taarifa juu ya ukubwa wa majeraha na muda gani watakuwa nje ya uwanja Pacome aliyeumia goti na Attohoula enka (kifundo cha mguu), itajulikana kesho baada ya kupata vipimo.
“Ni kweli Pacome na Attohoula walishindwa kumaliza mchezo kwa sababu ya kuumia ambapo mmoja aliumia goti na mwingine enka, kwa taarifa za daktari bingwa hadi saa 72 baada ya mchezo wetu dhidi ya Azam FC,” amesema Kamwe.
Kocha Msaidizi wa Azam FC, Youssouph Dabo, amesema mchezo ulikuwa wa ushindani na zimekutana timu mbili zenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao.
“Tulicheza mpira kwa ufanisi, tumeweza kuyatendea haki maboksi mawili, la mpinzani wetu na letu, tulicheza kwa kuwaheshimu Yanga kwa kuzuia ili wasipate nafasi ya kuongeza bao, baada ya kufunga la kwanza, lakini tutumie vizuri boksi lao kwa kupitisha mipira yote tulifanikiwa,” amesema Dabo.
Naye Fei Toto ambaye alikuwa mwiba mchungu kwa Yanga, amesema walifuata maelekezo na kucheza mechi hiyo kwa nidhamu kubwa kwa kuwaheshimu wapinzani wao.
“Yanga ni timu kubwa, lakini tulitaka kuonyesha kuwa na sisi ni wakubwa kwa kucheza mchezo wa kikubwa. Nina waheshimu Yanga timu iliyonitoa mbali hadi kujulikana kwa hali hiyo niliwaomba msamaha baada ya kuwafunga.
"Hilo si mimi tu, hata wachezaji Ulaya tunaona mchezaji anapoifunga timu iliyomtoa mbali na kumpa jina hufanya nilichokifanya mimi, sina tatizo na mtu, ninawapenda Yanga,” amesema Fei Toto.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED